24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yafafanua mradi wa umeme Kinyerezi II

2Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WIZARA ya Nishati na Madini imetoa ufafanuzi kuhusu mradi wa umeme wa Kinyerezi II na kusema kuwa bado haujaanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mawasiliano wa Serikali wa wizara hiyo, Badra Masoud, alisema Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Japan kuhusu mkopo wa masharti nafuu.

“Serikali ya Tanzania iliingia makubaliano na Serikali ya Japan ya mkopo wa masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 292 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 240 utakaojengwa na Kampuni ya Sumitomo kama mkandarasi wa “EPC contractor” na si kama mbia wa Serikali yaTanzania kama ilivyodaiwa.

“Mradi huo unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Tanesco na hakuna mwekezaji mwingine katika mradi huo. Hivyo si kweli kwamba Serikali ya Tanzania na Kampuni ya Sumitomo zinawekeza kwa ubia wa asilimia 40 (kwa Serikali ya Tanzania) na asilimia 60 kwa Sumitomo.

“Kwa maana hiyo hatutauziwa umeme utakaozalishwa na mradi huu kwani ni mali yetu na hakuna gharama yoyote ya ziada,” alisema Badra.

Alisema pamoja na hali hiyo, mradi huo bado haujazinduliwa na sasa upo katika maandalizi ya kuwekwa jiwe la msingi.

Akizungumzia kuhusu gharama za mradi huo, alieleza kuwa unatekelezwa kwa dola za Marekani milioni 344 sawa na Sh bilioni 740 zikiwa ni mkopo wa masharti nafuu wa asilimia 85 sawa na dola za Marekani milioni 292 na mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15 sawa na dola za Marekani milioni 52.

“Mwandishi wa habari hii amejaribu kufananisha uwekezaji huu na uwekezaji wa Tallawara Power Station ya Australia na kudai kwamba gharama yake ingekuwa ndogo kuliko gharama ya mradi huu.

“Kampuni ya Tallawara haijawahi kuomba au kuonyesha nia ya kuwekeza katika mradi wowote wa kufua umeme nchini. Pia ni muhimu ifahamike kwamba makubaliano ya mkopo huu yalikuwa yanakwenda sambamba na utekelezaji wa mradi wenyewe,” alisema Badra.

Aliongeza kwamba pamoja na kwamba gharama za uwekezaji wa mradi huo wa kwanza wa aina ya ‘Combined Cycle’ nchini zinawiana na gharama za miradi mingine ya aina hiyo duniani, gharama za uwekezaji zinaweza kutofautiana kutegemeana na mazingira ya nchi na nchi, teknolojia iliyotumika na aina ya mitambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles