24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Hatima ya Burundi EAC shakani

Rais-wa-Burundi-Pierre-NkurunzizaNA ELIYA MBONEA, ARUSHA

BUNGE la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), limeombwa kuiondoa nchi ya Burundi katika uanachama wa jumuiya hiyo na ile ya Umoja wa Afrika (AU) hadi hapo mgogoro wa kisiasa na kijamii utakapomalizika nchini humo.

Ombi hilo limewasilishwa mjini hapa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa Afrika, Donald Deya, alipowasilisha maombi ya mashirika sita yasiyo ya kiserikali kutoka EAC yaliyoomba kuzungumza na Bunge juu ya mgogoro wa Burundi.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Mambo ya Ndani ya Bunge na Usuluhishi wa migogoro ya EALA inayoongozwa na Mwenyekiti Abdullah Mwinyi, Deya alisema nchini Burundi bado kuna shida ya kisiasa na kuna Serikali iliyochaguliwa, lakini si halali kisheria.

Alisema pamoja na maombi ya kuondolewa kwa nchi hiyo, bado itaendelea kushiriki kwa karibu katika meza ya mazungumzo kwa ajili ya kutafuta mwafaka utakaowezesha kupatikana kwa amani na kuondoa shida zinazowakabili kwa sasa.

“Kitu cha msingi ambacho tunaliomba Bunge hili, litumie mbinu zote kuhakikisha Warundi wote wamefika mezani kwenye mazungumzo ya kutoa mwafaka wa shida yao. Na mbinu wanazoweza kutumia zipo nyingi,” alisema Deya na kuongeza:

“Sisi tunasema kwa sasa Serikali ya Burundi iwekwe ‘suspended’ (pembeni) kabisa kwenye uanachama wa Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ule wa Umoja wa Ulaya (AU),” alisema Deya.

Akiwasilisha maombi hayo ndani ya ukumbi wa Bunge uliopo Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mjini hapa, Deya alisema kumekuwapo na ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na kijamii huku baadhi wakiogopa na kuiona nchi hiyo inaweza kuteketea na kuingia kwenye mauaji ya kimbari.

“Kwa maoni yetu ukilinganisha mazungumzo ya utatuzi wa mgogoro wa Burundi na mazungumzo yaliyosaidia kuiondoa Kenya kwenye machafuko mabaya ya kisiasa mwaka 2008, utaona tofauti kubwa kabisa,” alisema Deya.

Akifafanua kuhusu mazungumzo yaliyoinusuru Kenya kutumbikia kwenye wimbi la mauaji zaidi, alisema aliyekuwa Mwenyekiti wa AU na Rais wa Ghana, John Kufor, aliiwezesha nchi hiyo kurejea kwenye amani tofauti na ilivyo kwa Burundi leo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge EALA, Mwinyi alisema kwamba maombi yaliyowasilishwa na mashirika hayo sita kupitia jopo la wanasheria wa Afrika yamesikilizwa na wajumbe wa kamati hiyo.

“Kuna mambo mengi wamependekeza, leo wajibu wetu Kamati ya Bunge ni kuyasikiliza na kutafuta ufafanuzi wa kina, ushahidi na baada ya hapo kamati itakaa kwa ajili ya kuyajadili na baadaye tutaandika ripoti na kuipeleka Bunge ili nalo lijadili na kutoa maazimio ya mapandekezo,” alisema Mwinyi na kuongeza:

“Sisi hapa hatuna dhamira ya kumtenga mtu wala kikundi au Serikali, dhamira yetu ni kusikiliza na kikubwa tunachokitafuta hapa ni suluhisho ili hatimaye tusitishe mauaji yanayotokea Burundi kwa pande mbalimbali.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles