NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
KOCHA aliyetupiwa virago juzi na uongozi wa Klabu ya Simba, Dylan Kerr, amesema hawezi kurudi nchini kwao hadi uongozi huo umlipe mishahara yake ya miezi miwili anayowadai.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kerr alisema hana shaka na maamuzi yao waliyoyaamua juu yake ya kuvunja mkataba, lakini kilichobaki ni wammalizie madai yake ili waachane kwa amani.
“Wameniahidi watanipa mishahara yangu leo (jana), mimi siondoki hadi watakaponipa sitaki kubakisha madeni nataka tuachane vizuri,” alisema.
Alisema atakapomalizana nao ataondoka kuelekea nchini kwao kwa ajili ya kuangalia muelekeo mwingine, kama atapata timu ya kuifundisha.
Alieleza kila timu ina mipango yake labda wameona haitatimia ndio maana wamechukua maamuzi hayo, hawezi kumlazimisha mwajiri wake aendelee kumpa mkataba kwani yeye ndio mwenye maamuzi.
“Naishukuru Simba na Watanzania wote kwa sapoti waliyonipa kwa kipindi nilichokuwepo hapa,” alisema.
Inadaiwa kocha huyo alikuwa akilipwa mshahara zaidi ya shilingi milioni 12 kwa mwezi, hivyo anawadai zaidi ya Sh milioni 24.
Kerr anaachana na Simba akiwa ameiongoza kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kucheza mechi 13, ikashinda nane, droo tatu na kufungwa michezo miwili.