30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Mayanja kurejesha soka la kitabu Simba

Jackson MayanjaNA MICHAEL MAURUS, ZANZIBAR

KOCHA msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja, amesema kuwa amekuja katika timu hiyo ili kurejesha soka lao la asili ambalo ni la kitabuni la pasi fupi fupi na za haraka, lakini pia kuwawezesha wachezaji kuwa na stamina ya kutosha pamoja na umakini wa hali ya juu.

Wachezaji wa Simba jana walionja joto ya jiwe, baada ya kuhenyeshwa na kocha huyo kwa kufanya mazoezi kwa dakika 140 kwenye Uwanja wa Amaan, visiwani hapa.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mayanja alisema Simba ina soka lake la asili ambalo kwa kipindi halijaonekana, hivyo uwepo wake katika klabu hiyo utasaidia kulirudisha.

“Simba ni timu kubwa ambayo ina utamaduni wake, nafahamu aina ya soka la Simba, ni soka la kuvutia. Niko hapa kuifanya kazi yangu kama ambavyo viongozi wa Simba wanategemea na ninawaahidi watu wa Simba sitawaangusha,” alisema.

Alisema iwapo aliweza kuifanya Kagera Sugar kuwa tishio enzi hizo, basi itakuwa ni zaidi kwa Simba iliyosheheni wachezaji wenye uwezo mkubwa, lakini ikiwa ni timu kubwa yenye kila aina ya nyenzo za kumwezesha kufanya kazi yake ipasavyo.

“Lakini ili niweze kufanikiwa katika hayo, nimelazimika kuanza na kuwajenga kisaikolojia wachezaji, lakini pia kurejesha morari na kila mmoja kufahamu thamani yake ya kuwa katika timu kubwa kama Simba,” alisema.

Mayanja jana alianza mazoezi yake saa 10:15 asubuhi na kumaliza saa 12:35 mchana, huku akiwatoa jasho nyota wa timu hiyo.

Katika mazoezi yake hayo, Mayanja alianza kwa kuwajengea wachezaji wake stamina kupitia mazoezi ya viungo yaliyodumu kwa dakika 15 kabla ya kuhamia katika kuchezea mpira.

Akizungumzia mazoezi ya kocha huyo, Nahodha wa Simba, Hassan Isihaka, alisema wameyafurahia akiamini yanaweza kuwasaidia kufanya vema kwenye mechi zao zijazo za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Alisema kocha huyo anaonekana kuwa makini zaidi na kazi yake, akiahidi wachezaji wote kumpa ushirikiano unaostahili ili aweze kutimiza malengo yake.

“Tumempokea vizuri kocha wetu mpya na tunaahidi kumpa ushirikiano pamoja na kufuata maelekezo yake,” alisema Isihaka ambaye ni beki wa kati wa kutumainiwa wa Simba.

Kikosi cha Simba kilichokuwa kimeweka kambi visiwani hapa tangu ilipotolewa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo fainali yake ilitarajiwa kufanyika jana kati ya Mtibwa Sugar na URA ya Uganda, inarejea Dar es Salaam leo jioni kuendelea na kambi yake.

Wachezaji wote wa timu hiyo walikuwapo kambini kasoro Abdi Banda, ambaye inadaiwa alirejea Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa vipimo kutokana na majeraha ya paja yaliyokuwa yakimkabili tangu wiki iliyopita, kwa mujibu wa daktari wa Simba, Gembe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles