WAKATI shinikizo la kimataifa juu ya hali ya Zanzibar likipamba moto, Rais Dk. John Magufuli, amekutana na aliyekuwa mgombea urais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo kwa saa 2.
Hali ya kisiasa ya Zanzibar, tayari inatajwa kuiathiri Tanzania kwa kusababisha ikose zaidi ya Sh trilioni 1 zilizokuwa zitolewe na Marekani, ikiwa ni sehemu ya fedha za msaada wa Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC).
Taarifa iliyotolewa na Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema mazungumzo hayo yametokana na maombi ya Maalim Seif ya siku nyingi na kuwa yalihudhuriwa pia na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
“Viongozi hawa kwa pamoja wamejadili hali ya kisiasa Zanzibar na wamefurahishwa na hali ya usalama na utulivu inayoendelea. Rais Dk. Magufuli amewapongeza Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Maalim Seif na viongozi wote wanaoshiriki katika mazungumzo ya kuleta hali ya uelewano Zanzibar.
“Rais Magufuli pia amewapongeza na kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kudumisha amani na utulivu, wakati mazungumzo baina ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yakiendelea huko Zanzibar,” ilisema taarifa ya Ikulu.
Taarifa hiyo, ilisema Maalim Seif amemweleza Dk. Magufuli juu ya hali ya siasa Zanzibar, huku kiongozi huyo wa Jamhuri ya Muungano akimshukuru kwa taarifa yake aliyosema ni nzuri na akamsihi waendelee na mazungumzo hadi mwafaka upatikane.
Ilisema majadiliano yanayoendelea yanatoa fursa ya kudumishwa kwa utulivu na sifa njema ya Tanzania.
“Wote kwa pamoja wamewaomba wananchi waendelee kuwa watulivu ili kutoa nafasi ya majadiliano yanayoendelea kufikia hatma njema. Wameelezea matumaini yao kuwa vyama vya CCM na CUF haviwezi kushindwa kupata suluhu ya mgogoro huo,” ilisema taarifa hiyo.
Maalim Seif pia amekutana takribani mara saba na Dk. Shein, huku mazungumzo yao yakiwa ni siri kubwa.
MAPEMA BAADA YA UCHAGUZI
Baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi visiwani humo, Serikali ya Uingereza na ile ya Ireland Kaskazini zilipinga uamuzi huo.
Serikali hizo zilisema hazioni sababu ya kufutwa matokeo hayo, baada ya waangalizi wa kimataifa kufurahishwa na uchaguzi ulivyofanyika kwa amani.
UMOJA WA MATAIFA
Oktoba 29, mwaka huu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alipongeza Tanzania kwa kufanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu huku akionyesha masikitiko yake juu ya hali ya Zanzibar.
Taarifa ya UN iliyotolewa kwa vyombo vya habari, ilisema Ki-moon anataka hali ya Zanzibar ichukuliwe kwa umakini na imalizike kwa amani. Ilisema mashauri yote yafuate sheria na yajadiliwe katika hali ya uwazi.
Ban Ki-moon alitaka pande zote zinazohusika na mgogoro huo kuwa tulivu na ziwe makini katika kutoa matamko ili yasivuruge hali ya amani.
JK NA MAALIM SEIF
Novemba 4, ikiwa ni siku moja kabla Rais Jakaya Kikwete hajakabidhi madaraka kwa Rais Dk. Magufuli, alikutana na Maalim Seif Ikulu Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo kwa takriban saa moja.
Licha ya kuwa haikuelezwa juu ya kile kilichokuwa kiini cha mazungumzo hayo, ilibainishwa kuwa lengo kuu lilikuwa hali ya usalama visiwani humo ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikionekana tete zaidi.
MAANDAMANO
Katika kuendelea kushinikiza hali ya usalama visiwani humo, baadhi ya Wazanzibari wanaoishi nchini Uingereza, walidaiwa kufanya maandamano kutaka Uingereza iingilie kati na kuweka shinikizo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili mshindi wa uchaguzi wa urai atangazwe na kuapishwa.
Baadhi ya picha kwenye mitandao, zilionyesha sehemu ya waandamanaji wakiingia Mtaa No. 10 Downing ambako kuna Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, kukabidhi barua yao.
Nao Wazanzibari wanaoishi nchini Sweden walifanya maandamano jijini Stockholm Desemba 14, kutaka Bunge la nchi hiyo (Riksdag) na Serikali kuibana Tanzania ili iheshimu uamuzi wa wananchi wa Zanzibar walioufanya kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba 25.
MABALOZI WA CHINA, UAE
Desemba 9, Maalim Seif alikutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini, Dk. Lu Youqing katika ofisi za ubalozi wa China, Oysterbay Dar es Salaam.
Siku hiyo hiyo, Maalim Seif alikutana na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Abdallah Ebrahim Al-Suwid, katika ofisi za ubalozi huo, Masaki, Dar es Salaam.
Mazungumzo yote hayo yalilenga kueleza hali ilivyo visiwani humo na kutaka kuongeza shinikizo la kutafuta suluhu.
SHINIKIZO LA MCC
Kutokana na shinikizo la ndani kwenye jumuiya za kimataifa, Bodi ya MCC iliyokaa Desemba 16, kuidhinisha fedha hizo, iliinyima Tanzania dola za Marekani milioni 472 (takribani Sh trilioni 1.3).
Taarifa ya MCC ilisema: “Bodi iliahirisha kupiga kura kwa Tanzania. Ilijadili wasiwasi unaoendelea juu ya hali ya Zanzibar pamoja na matumizi ya sheria ya mtandao.”
Kutokana na hali hiyo, Tanzania itajadiliwa tena na bodi hiyo mwaka 2016 kama kutakuwa na mabadiliko kwenye nyanja hizo.