LUANDA, ANGOLA
RAIS wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Uganda Yoweri Museveni wamesaini makubaliano ya kubadilishana wafungwa, baada ya mazungumzo ya upatanishi yaliyoongozwa na Angola mjini Luanda juzi.
Hakukuwa na taarifa zaidi kuhusu idadi ya wafungwa watakaoachiwa, wala muda wa kuachiwa kwao baada ya tukio hilo adhimu.
Marais hao, Kagame na Museveni waliwahi kuwa washirika wakubwa, lakini urafiki wao umegeuka uhasama, huku kila nchi ikiituhumu nyingine kuendesha ujasusi dhidi yake, na kuyasaidia makundi ya waasi yanayonuiya kuiangusha serikali yake.
Katika mkutano wa juzi ambao ulimshirikisha pia rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi, Kagame na Museveni walikubaliana kukutana tena Februari 21 mwaka huu, kwenye mpaka wa Gatuna kati ya nchi zao.
Mwezi Agosti mwaka jana nchi hizo zilisaini makubaliano ya kuboresha uhusiano wa kisiasa na wa kibiashara, lakini hakukuwa na maendeleo ya maana hali inayoonyesha kuwa kila mmoja alikuwa na hofu na mwenzake.