Na MOHAMED KASSARA
KIKOSI cha Yanga leo kitashuka dimbani kusaka pointi tatu ugenini dhidi ya Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Yanga inashika nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 13 baada ya kucheza michezo sita, ikishinda minne, sare moja na kupoteza mmoja.
Wanajagwani hao watashuka dimbani wakitoka kuichapa JKT Tanzania mabao 3-2 katika mchezo wa mwisho uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Alliance wanaokutana nayo, inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo 12, ikishinda minne, sare tano na kupoteza mitatu.
Vijana hao wa Alliance watashuka dimbani wakitoka kupokea kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Azam katika mchezo wao wa mwisho uliochezwa Jumatatu kwenye uwanja huo.
Yanga itaishukia Alliance ikijivunia rekodi nzuri za Kaimu kocha Mkuu wao, Charles Mkwasa, ambaye tangu akabidhiwe mikoba ya kukiongoza kikosi hicho hajapoteza mchezo wa ligi.
Mkwasa ambaye amechukua jukumu hilo baada ya Mwinyi Zahera kutimuliwa, ameiongoza Yanga kuvuna jumla ya pointi katika michezo dhidi ya Ndanda na JKT Tanzania.
Katika michezo hiyo, kikosi hicho kimeonekana kuimarika, hasa kwenye safu ya ushambuliaji, baada ya kupachika mabao manne, ikiwa ni wastani wa mabao mawili kila iliposhuka dimbani.
Kabla ya hapo, kikosi hicho chini ya Zahera kilikuwa kimetikisa nyavu za wapinzani mara tano katika michezo minne.
Hata hivyo, Yanga bado inakabliwa na changamoto katika eneo la ulinzi, ambapo katika michezo yake sita imeruhusu wavu wao kuguswa mara sita, ikiwa ni wastani wa kupitisha bao moja kila mechi.
Yanga itaingia uwanjani kuikabili Alliance ikijivunia rekodi yake nzuri ya kuvuna pointi zote sita dhidi ya timu hiyo walipokutuana msimu uliopita, ikianza kushinda mabao 3-0 jijini Dar es Salaam, kabla ya kuichapa bao 1-0 katika mchezo mzunguko wa pili.
Akizungumza
na MTANZANIA jana, Mkwasa alisema
kikosi chake kipo sawa na morali ni kubwa kuhakikisha wanapata pointi tatu
muhimu katika mchezo huo.
“Mchezo utakuwa mkubwa
na mgumu, hivyo tutaingia uwanjani tukiwa na tahadhari kubwa ili kupata matokeo
chanya.
“Tumejipanga vilivyo kuhakikisha tunapambana kadiri ya uwezo wetu kushinda ili kujiongezea pointi. Tunajua tuko nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi, hata hivyo bado tuna viporo vingi, hivyo kazi iliyo mbele yetu ni kuvitafuna ili kwenda juu zaidi,” alisema Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Yanga.
Kwa Upande wake, Kocha Msaidizi wa Alliance, Habib Kondo, alisema kikosi chake kimejipanga vema kuichapa Yanga ili kurudisha pointi zao tatu walizopoteza katika mchezo uliopita.
“Tumejipanga kuja kivingine kabisa katika mchezo huo, tutabadili staili yetu kidogo. Nimefanya hivyo kutokana na namna nilivyofuatilia Yanga wanavyocheza na nimekuja na mikakati kabambe kuhakikisha tunashinda mchezo huo ili kulipa kisasi cha kupoteza mchezo wa Azam,” alisema Kondo.