Mwandishi wetu , Kigoma
TIMU ya Simba jana ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa katika mchezo wa kirafiki uliochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Ushindi ni wa pili kwa Simba katika mchezo wa kirafiki baada ya Jumamosi iliyopita kuibuka na matokeo kama hayo dhidi ya Bandari ya Kenya, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo wa jana bao pekee la Simba lilifungwa dakika ya 56 na kiungo wa timu hiyo, Sharaf Shiboub ambaye aliunganisha kwa kichwa krosi ya Said Ndemla.
 Kipindi cha kwanza timu hizo zilionekana kushambuliana kwa zamu huko kila moja ikihitaji kupata bao la kuongoza, lakini milango ilikuwa migumu kufunguka.
 Mchezo huo uliohudhuriwa na mashabiki wengi, Kocha wa Simba, Patrick Aussems alifanya mabadiliko kwa kumtoa Francis Kahata na nafasi yake kuchukuliwa na Shiboub na kupeleka kilio kwa Mashujaa inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.Â
Simba wanatarajia kushuka dimbani kesho kucheza na mabingwa wa Burundi Aigle Noir, ukiwa ni mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika.
Wekundu wa Msimbazi wanajiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC, utakaochezwa kuchezwa Oktoba 23 mwaka huu, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.