Wananchi waonyesha hofu ya samaki kutoweka

0
532

Nyemo Malecela -Kagera

WANANCHI wa Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera wameziomba mamlaka zinazosimamia mazao ya majini mkoani Kagera kuingilia kati kuzuia shughuli za uvuvi katika Ziwa Ikimba ili kutoa fursa ya samaki aina ya sato kuzaliana na kukua.

Akizungumzia hilo mkazi wa Kitongoji cha Ikimba Area, Sued Rashid alisema kwa sasa hakuna uwezekano wa kupata samaki mwenye uzito wa kilo mbili katika ziwa hilo.

“Lakini kwa uvuvi unaoendelea sasa ili familia iweze kupata samaki wa kutosha mlo mmoja, lazima ipate samaki aina ya sato wasiopungua wanne au watano wakati samaki hao wakikua katika kiwango kinachotakiwa wanaweza kutumika kwa milo miwili kwa siku tatu,” alisema.

Sued alisema kwa sasa wanakijiji wanaotegemea ziwa hilo wanakosa samaki aina ya sato wenye viwango vinavyostahili kutokana na ziwa hilo kukumbwa na uvuvi haramu.

“Kwa umri wangu tangu nikiwa mdogo tulikuwa tukivua sato na kambale na jamii nyingine ya samaki ambazo zinaridhisha kwa ukubwa, lakini sasa hivi kwa upande wa kambale hamna shida ila kwa upande wa samaki jamii ya sato tunaelekea kuipoteza kabisa katika ziwa hilo.

“Sato wanaovuliwa katika ziwa hilo ni wadogo mno kutokana na nyavu zinazotumika kuvulia hazikubaliki kisheria, ikiwezekana mamlaka zinazosimamia uvuvi ziielimishe jamii kulima visima vya kufuga samaki ili kupunguza uvuvi katika ziwa hilo ili samaki waweze kukua,” alisema Sued.

Mwananchi huyo alisema kuwa mwaka 2017/18 mamlaka zinazosimamia uvuvi zilisitisha uvuvi katika ziwa hilo kwa kipindi cha miezi sita na kusababisha samaki kukua na kuongezeka, jambo lililofanya wavuvi kukua kiuchumi kutokana na kuvua samaki wakubwa wanaouzika bila woga kwa jamii.

Ofisa Mifugo kwa niaba ya Ofisa Mifugo na Uvuvi wa Wilaya ya Bukoba, Happnes Matiku alisema katika kudhibiti uvuvi haramu doria zinafanyika na nyavu haramu zinazokamatwa zinachomwa moto.

“Kila mwalo katika ziwa la Igabilo, Malehe, Kemondo na Ikimba zilizopo katika Halmashauri ya Bukoba wapo wawakilishi maofisa uvuvi (BMU) wanashirikiana na watendaji kudhibiti uvuvi haramu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here