Sheila Katikula -Mwanza
BAADHI ya wamiliki wa mitumbwi na wavuvi wa Mwalo wa Butuja, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani kuimarisha ulinzi na usalama Ziwa Victoria.
Hii ni baada ya kuwepo kwa madai ya kuvamiwa, kuuawa na kunyang’anywa samaki baadhi ya wavuvi wakiwemo wa mwalo huo wanaofanya shughuli zao Ziwa Victoria na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, mfanyabiashara wa samaki Mwalo wa Butuja, mmiliki wa mitumbwi ya MV. Tunda, Abel Kaitira, alisema wanalia na vitendo hivyo vya ukatili kwani wameishatoa taarifa ngazi za chini, lakini hakuna kilichofanyika.
“Watu wanakufa, mali zinateketea, tunazidi kuumia, sisi tutakuwa katika mazingira gani? Ili tukomeshe vitendo hivi tunaomba Waziri wa Mambo ya Ndani kutusaidia kuwabana baadhi ya askari wanaowanyang’a wavuvi samaki bila kufuata utaratibu.
“Ikiwezekana Serikali kupitia wizara hiyo iweke operesheni ya jeshi ambayo itasaidia kuimarisha ulinzi na usalama ziwani, huku wavuvi wakivua kwa amani.
“Kuna tetesi kuwa wapo baadhi ya wavuvi ambao ni majambazi wanaingia majini na kufanya vitendo hivyo, tusaidiwe ili waweze kupatikana hata kama kuna matajiri wanahusika,” alisema Kaitira.
Mwenyekiti wa Utunzaji wa Viumbe hai ndani ya mita 60 mwambao mwa Ziwa (BMU), Mwalo wa Butuja, Dickson Maila, alisema ni vema Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza doria ili kuimarisha ulinzi na usalama ziwani kwani zilizopo ni chache, huku wavuvi wakipatiwa elimu ya kutambua mipaka ziwani inayotenganisha nchi moja na nyingine pamoja na matumizi ya dira ili kutambua mwelekeo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu, alisema jambo la ulinzi na usalama ziwani ni mtambuka, hasa wa vyombo vya ulinzi na usalama na anashukuru vyombo hivyo vinafanya kazi kubwa na nzuri.
“Lakini bado tunaendelea katika kuhimizana na kufanya zaidi ili kuwasaidia hawa Watanzania wanaokutana na madhila mbalimbali wawapo majini,” alisema.