RC awataka viongozi Gairo kufanya kazi bila tabaka

0
767

Ashura Kazinja -Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Loata ole Sanare, amewataka viongozi wa Halmashauri ya Gairo kufanya kazi na watumishi kwa karibu bila kuweka matabaka, baada ya kupokea ujumbe mfupi wa simu ukieleza mambo kutokuwa shwari ndani ya halmashauri hiyo.

Sanare alitoa maagizo hayo jana wilayani Gairo, wakati akizungumza na watumishi hao, kwa lengo la kusalimia na kujitambulisha akiwa njiani kutoka Dodoma kikazi.

Aliwataka viongozi hao kuacha kuweka matabaka baina yao, watumishi na wananchi ili kuimarisha umoja miongoni mwao.

Sanare alisema amepokea ujumbe mfupi wa simu (SMS) kutoka kwa wananchi na watumishi wakieleza  mambo hayako shwari ndani ya halmashauri hiyo, hivyo kuwataka viongozi hao kuhakikisha wanaweka mambo sawa na kufanya kazi zao kwa ushirikiano.

“Ni vyema tuwasaidie watumishi kufanya kazi zao vizuri, tusije tukajaribu kuwa na matabaka ndani ya utumishi, ni hatari sana, ushirikiano katika kazi ni mzuri,” alisema Sanare.

Alitumia nafasi hiyo kukemea tabia ya kutumia fedha za makusanyo ya ndani ya halmashauri kabla hazijaingizwa benki katika akaunti ya halmashauri kwa kuwa huo si utaratibu wa Serikali, na kuagiza matumizi ya fedha hizo kufanyika baada ya kuwa zimeshaingizwa katika akaunti.

Aliomba ushirikiano kutoka kwa watumishi wa halmashauri hiyo na ofisi yake pamoja na kamati ya ulinzi na usalama za mkoa na wilaya, ili kuondoa sintofahamu iliyopo katika halmashauri hiyo.

 “Nini hiki kinachoendelea ndani ya halmashauri, ninajua kuna mambo ya ovyo yanaendelea kufanyika, hata hivyo niwahakikishie yako mwishoni kuisha, na itabidi kuvumilia pale nitakapochukua hatua za kinidhamu kwa baadhi ya watumishi wasiowajibika ipasavyo,” alisisitiza Sanare.

Sambamba na kutoa onyo kwa viongozi na watumishi, pia hakuacha kuwapongeza watumishi wanaofanya kazi zao kwa bidii, uadilifu na uwajibikaji mkubwa, na kuwataka kuendelea kujituma na kujitoa kwa mkoa na taifa kwa ujumla.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Morogororo, Emmanuel Kalobelo, aliwataka viongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanasimamia kwa ukamilifu ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi yake.

Alisema usimamizi wa miradi ya maendeleo bado ni changamoto kwa halmashauri hiyo, na kusema ataomba kupewa taarifa ya miradi yote, ikiwemo yenye changamoto katika utekelezaji wake, aliyoiita ni chechefu ili aweze kuifanyia kazi.

Aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kutoa taarifa mbalimbali za kiserikali katika ofisi yake zilizo sahihi na kwamba zitolewe kwa wakati, kwani lengo limekuwa halifikiwi kutokana na kuwa na sababu ambazo pengine zimekuwa hazitolewi kwa wakati.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao, aliwataka watumishi wa Serikali wilayani humo kusimamia kikamilifu.

Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe, alisema kuna mwelekeo mzuri wa makusanyo ya ndani ya mapato ya halmashauri kutokana na uwepo wa machimbo ya madini ya dhahabu ya Kilama, na kutumia fursa hiyo kuomba mahusiano baina ya ofisi yake na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuboreshwa.

Watumishi wa halmashauri hiyo walimwomba Sanare mbali na changamoto nyingi, waliomba ufumbuzi wa haraka wa changamoto ya kukosekana kwa umoja miongoni mwao.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here