NA VALERY KIYUNGU, DAR ES SALAAM
MWANAMUZIKI wa siku nyingi wa muziki wa dansi nchini, ambae alikuwa na Bendi ya Wazee Sugu inayoongozwa na nguli King Kikii, Kasongo Mpinda ‘Clayton’, amefariki dunia jana jioni.
Marehemu kabla kufikwa na umauti alikuwa mwanamuziki muimbaji wa kutumainiwa kwenye bendi hiyo kongwe, inayotamba na wimbo wa Kitambaa Cheupe. Mwili wake umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam.
Kiongozi wa bendi ya Wazee Sugu King Kikii, amethibitisha kufariki kwa mwanamuziki huyo, akieleza ameshutushwa na taarifa za kifo hicho.
‘Ni kweli Kasongo amefariki kwani hata mimi nimepigiwa simu muda si mrefu, nilikuwa naye katika ziara ya Dodoma ambapo tumerejea siku si nyingi, kwa kweli nimesikitisshwa mno
,” alisema.
Kasongo Mpinda alizaliwa wakati Vita Kuu y Pili ya Dunia ikikaribia kumalizika, anatoka katika ukoo wa ki Chifu, baba yake alikuwa Chifu akiitwa Chifu Kasongo huko Kasai, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Ni mtoto wa kwanza kati ya wanane aliyezaliwa Februari 02, 1945, katika mji wa Lubumbashi jimbo la Shaba huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Aliingia Tanzania mwaka 1979, baadhi ya bendi alizowahi kupigia ni M.K Group ambayo iliwahi kushinda tuzo kupitia wimbo wake wa ‘Uwajibikaji’ katika shindano la Top Ten Show mwaka 1988.
Uwajibikaji ilikuwa ni kauli mbiu ya rais wa awamu ya pili, Alhaj Alli Hassan Mwinyi kwa watanzania akiwataka kuwajibika katika kazi ipasavyo.