Theresia Gasper,Dar es salaam
MSHAMBULIAJI Meddie Kagere ameendelea kutakata, baada ya jana kuifungia Simba bao moja kwenye ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kagere tayari amefunga mabao mawili msimu huu, baada ya kuifungia Simba bao pekee ilipoitandika JKT Tanzania mabao 3-1, katika mchezo wa kwanza uliopigwa pia kwenye uwanja huo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika Simba na Simba kwenda mapumziko zikiwa nguvu sawa, baada ya kufungana bao 1-1.
Kagere alifunga bao la kuongoza la Simba dakika ya 18, baada ya kumalizika mpira uliopigwa na Sharaf Shiboub.
Lakini shangwe za mashabiki wa Simba hazikudumu muda mrefu kwani Riphat Msuya aliisawazishia Mtibwa Sugar kwa kufunga bao dakika ya 21, akiunganisha kona iliyochongwa na Issa Rashid maarufu Baba Ubaya.
Kipindi cha pili, kila upande ulizidisha kasi ya mashambulizi kwa lengo la kusaka mabao zaidi.
Dakika ya 63, Kocha wa Simba, Patrick Auusems alimtoa Hassan Dilunga na kumwingiza Miraj Athuman kabla ya Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila kumtoa Haruna Chanongo dakika ya 67 na kumwingiza Omar Hassan.
Dakika ya 68, Miraj aliiandikia Simba bao la pili kwa shuti kali, baada ya kuunganisha pande la Shiboub.
Dakika ya 79, Aussems alimtoa Clatous Chama na kumwingiza Fransis Kahata.
Mtibwa
ikamtoa Ismail Mhesa dakika ya 81 na kuingia Abdul Haule kabla ya Rashid kutoka
dakika ya 85 na kuingia Henry Joseph.
Dakika ya 89 alitoka Shoboub na kuingia Jonas Mkude.
Pamoja na mabadiliko ya kila upande, dakika 90 zilikamilika kwa Simba kuchomoza na ushindi wa mabao 2-1.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, wenyeji Costal Union waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC.
Mabao ya Coast yalifungwa na Shabaan Idd dakika ya 62 na Ayub Lyanga dakika ya 75.