Wadhamini wanne waipa Alliance FC milioni 400

0
677

Damian Masyenene, Mwanza

KLABU ya Alliance FC ya jijini Mwanza imetangaza kuingia udhamini wenye thamani ya Sh. milioni 400 utakaotolewa na wadhamini wanne kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Udhamini huo ulitangazwa jana jijini Mwanza na Makamu Mwenyekiti wa Alliance, Nyaitati Stephano wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Njaitati aliwataja wadhamini hao ni Benki ya Access, Kampuni ya ujenzi ya Emirate Aluminium Profile, Maji ya Mwanza na Shule za Alliance.

Nyaitati alisema shule za Alliance zimechangia asilimia 50 ya udhamini huo, huku Access ikitoa asilimia 20, maji ya Mwanza asilimia 15 sawa na Kampuni ya Emirate.

Nyaitati alisema bajeti ya klabu yao kwa mwaka ni Sh bilioni 1, hivyo udhamini huo wa Sh milioni 400 pamoja na ule wa Vodacom(wadhamini wa Ligi Kuu) na Kampuni ya Azam Media,  utawasaidia kwa kiasi kikubwa kukidhi mahitaji ya timu yao.

Meneja Mauzo wa Emirate Aluminium Profile, Issa Maheda alisema sehemu ya mkataba waliouingia utaanzisha tuzo ya mchezaji bora wa mwezi atakayeteuliwa na benchi la ufundi na kupendekezwa na wachezaji wenzake, kisha kupigiwa kura na mashabiki wa klabu  hiyo.

“Mchezaji bora wa mwezi atapewa Sh 300,000 na tuzo, pia tumejikita kuwasaidia usafiri kwa kutoa mafuta katika safari zote za timu, vile vile tutakuwa tunatoa fedha kwa timu kuiwezesha katika mipango yake.

Tumeamua kuwekeza katika soka na hii ni timu ya kwanza kuidhamini,” alisema.

Ofisa Mwandamizi Masoko wa Access, Sijaona Malosha alisema mvuto ilionao Alliance ndio kitu kilichowashawishi kuingia nao mkataba wa udhamini.

“Tumevutiwa na menejimenti yao pamoja na filosofia ya kutengeneza vipaji, kuanzia ngazi ya chini, tumeamua kuwekeza kwenye michezo na tutazidhamini Alliance FC na Alliance Girls, wanajiamini na wanao uwezo wa kubeba ubingwa msimu huu,” alisema.

Alliance FC itashuka dimbani kesho Uwanja wa Nyamagana kuumana na Kagera Sugar katika mwendelezo wa Ligi Kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here