MANCHESTER, ENGLAND
BAADA ya timu ya Manchester United kukubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Crystal Palace juzi, kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer amedai hana furaha kuona wachezaji wake wanashindwa kufunga mikwaju ya penalti.
Huo ulikuwa ni mchezo wa pili tangu kufunguliwa kwa michuano ya Ligi Kuu England kwa Manchester United kukosa mikwaju ya penalti.
Wiki moja iliopita katika mchezo dhidi ya Wolves, United ilikosa penalti ambayo ilipigwa na kiungo wao Paul Pogba lakini mlinda mlango wa Wolves aliicheza na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Mchezo wa juzi dhidi ya Crystal Palace, United walikosa penalti kupitia kwa mshambulia wao Marcus Rashford na kuifanya timu hiyo ikubali kichapo hicho kwenye uwanja wa nyumbani.
Pogba na Rashford ni wachezaji ambao walichaguliwa kwenye kikosi kwa ajili ya kupiga penalti inapotokea, lakini baada ya Pogba kukosa lawama zilikuwa nyingi kutoka kwa mashabiki ambapo walimtaka mwalimu kufanya mabadiliko awe anapiga Rashford, lakini baada ya Rashford kushindwa na yeye kocha huyo amedai hana furaha.
“Michezo miwili tumeshindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji kukosa penalti ni jambo la kushangaza sana hasa kwenye uwanja wa nyumbani.
“Kwa upande mwingine wapinzani wamefunga mabao rahisi sana hii inaonesha safu ya ulinzi ilikosa maelewano, lakini safu ya ushambuliaji ilitengeneza nafasi nyingi ila walishindwa kuzitumia.
“Tuliweza kuumiliki mchezo, lakini hatukuweza kufanya hivyo kwa kipindi chote hasa katika dakika tano za mwisho na kuwafanya wapinzani watambe mbele ya uwanja wetu,” alisema kocha huyo.
Hata hivyo, kocha huyo aliwatupia lawama waamuzi kwa kushindwa kutenda haki katika baadhi ya matukio ya upande wao.
“Ninaamini tulitakiwa kupata penalti nyingi katika dakika 45 za kipindi cha pili ambapo Rashford aliangushwa kwenye eneo la hatari, lakini kitu cha kushangaza ni kwamba mwaamuzi hakufanya lolote, alikosa umakini,” aliongeza kocha huyo.