22.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Kim asimamia jaribio la makombora mawili

PYONGYANG, KOREA KASKAZINI

KOREA Kaskazini imeripotiwa kufanya jaribio la kurusha makombora mawili ya masafa mafupi baharini.

Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Korea Kusini.

Jaribio hilo ni la saba kutekelezwa tangu Korea Kaskazini ilipomaliza mpango wake wa miezi 17 wa kusitisha majaribio yoyote ya silaha zake.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha taifa hilo, KCNA jana, jaribio hilo lilisimamiwa na Rais Kim Jong Un.

KCNA ilisema kwamba lilikuwa jaribio la kombora kubwa ambalo liliundwa hivi karibuni.

Kim alilitaja kombora hilo kuwa silaha nzuri, huku akilishukuru kundi la wataalamu waliounda makombra hayo.

Maofisa wa kijeshi walisema makombora hayo yalirushwa saa 12.45 na saa 1.02 kwa muda wa Korea Kaskazini kutoka mji wa Mashariki wa Sondok, kusini mwa Mkoa wa Hamgyong.

Walisema kwamba makombora hayo yalirushwa umbali wa kilomita 380 na urefu wa kilomita 97 kabla ya kuanguka katika Bahari ya Japan, pia ikijulikana kama Bahari ya Mashariki.

“Jeshi letu linachunguza hali ilivyo iwapo majaribio zaidi yatafanyika huku tukijiandaa kukabiliana na athari zozote zinazoweza kujitokeza,” alisema mkuu wa jeshi wa Korea Kusini.

Waziri wa Ulinzi wa Japan, Takeshi Iwaya alithibitisha kombora hilo halikuanguka katika maji ya Japan, lakini akataja kuwa ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa (UN).

Pyongyang tayari imeonyesha na kueleza kukasirishwa na mazoezi ya kijeshi ya pamoja ya Marekani na Korea Kusini ambayo yamekuwa yakiendelea.

Korea Kaskazini imeyataja kuwa maandalizi ya vita na kusema kwamba yanakiuka makubaliano waliyoafikiana na Rais wa Marekani, Donald Trump na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in.

Marekani na Korea Kusini zimekataa kufuta mazoezi hayo na kwamba wameyafanya kuwa ya kiwango cha juu.

Katika taarifa ya Rais siku ya Jumamosi, Korea Kusini ilitoa wito kwa Korea Kaskazini kutoongeza wasiwasi wa kijeshi uliopo huku akisisitiza mpango wao wa mazungumzo na Marekani kwamba utaendelea.

Mazungumzo ya kutounda silaha za kinyuklia yamekwama tangu mkutano wa ana kwa ana kati ya Trump na Kim kugonga mwamba Februari mwaka huu.

Juni mwaka huu, viongozi hao wawili walikutana eneo la mpakani kati ya mataifa hayo ya Korea na kukubaliana kuendelea na mazungumzo.

Akizungumza baada ya majaribio hayo mawili, Rais Trump alisisitiza kwamba ana uhusiano mzuri na Kim ambaye anasema kuwa amekuwa mkweli kwake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles