Theresia Gaper -Dar es salaam
NAHODHA msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Erasto Nyoni, amesema alichagua kupiga penalti ya kwanza katika mchezo na Kenya ili kuwapa moyo wenzake.
Katika mchezo huo wa marudiano wa kufuzu michuano za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), Stars ilishinda iliibuka kidedea ikishinda kwa penalty 4-1, hivyo kufanikiwa kusonga mbele.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kasarani, Kenya, waliingia katika penalti baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90 na ule wa kwanza uliopigwa Dar es Salaam.
Akizungumza na MTANZANI, Nyoni, alisema Watanzani wanatakiwa kuendelea kuisapoti timu yao ili ifanye vizuri katika hatua inayofuata.
“Nimefurahi sana timu yetu kusonga mbele, hali hii imezidi kutupa morali ya juu, ujue nilijitoa kwenda kupiga penalti ya kwanza ili kuwatoa hofu wadogo zangu na ilifanikiwa kwani walipiga penalti zote bila wasiwasi,”alisema.
Alisema hawajaishia hapo, wataendelea kupambana katika mechi zijazo na kufanya vizuri zaidi.
Naye John Bocco, alisema ushindi waliopata ni kwa Watanzania wote, hivyo wanajipanga kwa mechi inayokuja dhidi ya Sudan waweze kufanya vizuri.
“Tunashukuru Watanzania waliweza kujitokeza katika mchezo huu japo walikuwa wachache lakini walishangilia kwa nguvu zote na kutupa morali ya kupata ushindi na kusonga mbele,” alisema.