Mwandishi wetu-Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amekutana na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alipokwenda kutoa pole nyumbani kwa marehemu Meja Jenerali mstaafu Albert Mbowe, aliyefariki dunia Jumapili iliyopita Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam.
Alienda nyumbani kwa marehemu Salasala, Dar es Salaam jana kukutana na familia ikiongozwa na Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema pamoja na kutia saini kitabu cha maombolezo, Rais Magufuli aliungana na familia hiyo katika sala ya pamoja ya kumwombea marehemu.
Baada ya sala hiyo, Rais Magufuli aliitaka familia hiyo iendelee kuwa na umoja kama ilivyokuwa wakati wa uhai wa Meja Jenerali mstaafu Mbowe na kumtanguliza Mwenyezi Mungu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo, alisema pamoja na kustaafu, Meja Jenerali Mbowe alikuwa mshauri wa karibu wa jeshi.
Alisema katika utumishi wake wa miaka 36 na siku 27 jeshini, Meja Jenerali mstaafu Mbowe, alitoa mchango mkubwa katika masuala ya usimamizi wa fedha.
Meja Jenerali mstaafu Mbowe, alizaliwa Januari 1953, alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1973 na alistaafu utumishi jeshini mwaka 2009.