24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Kangi kupambana biashara usafirishaji binadamu

Christina Gauluhanga -Dar es salaam

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, ametoa onyo kali na kuahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaojihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu huku akitaja mikoa kumi inayoongoza kwa utumikishwaji wa kazi za ndani.

Pia amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuwarejesha vijana watatu akiwamo mlemavu mmoja waliopo nchini Kenya, ambao wamebainika kuchukuliwa na kupelekwa nje ya nchi kwa lengo la kutumikishwa kama ombaomba wa fedha mitaani.

Hayo aliyasema jana Dar es Salaam katika maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Kupinga Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu.

Kangi alisema usafirishaji wa ndani ya nchi ndio unaoongoza nchini na waathirika wakubwa ni watoto, vijana wenye umri kati ya miaka 13 hadi 24.

Alisema wanaoingia katika mkondo huo wa biashara haramu huahidiwa kupatiwa kazi za ndani, kulea watoto, saluni, nyumba za kuuza pombe, kuchunguza au kuhudumia ng’ombe au kuishi na anayemchukua kwa malipo mazuri.

“Matokeo yake wengi hawapelekwi walikoahidiwa na kubwa zaidi hawapewi malipo, huku wengine wakipewa kiduchu tofauti na walichoahidiwa ukilinganisha na aina ya kazi wazifanyazo,” alisema.

Aliitaja mikoa iliyoathiriwa na biashara hiyo ni Dar es Salaam, Mwanza, Kigoma, Arusha, Geita, Singida, Dodoma, Shinyanga, Tanga na Morogoro.

Lugola alisema katika kipindi cha mwaka 2016/19 walifanya upelelezi wa matukio ya usafirishaji haramu wa binadamu 50 dhidi ya watuhumiwa 76.

Alisema watuhumiwa 60 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kulipa faini au kutumikia adhabu gerezani katika kipindi hicho.

Lugola alisema kati ya watuhumiwa hao, wanaume ni 53 na wanawake saba.

Akizungumzia usafirishaji binadamu kwenda nje ya nchi, hususan India na Oman kwa ahadi ya kazi na fedha nzuri, alisema wanatoka Dar es Salaam, Tanga, Dodoma na Kondoa na wachache mikoa mingine.

Alisema waathirika wakubwa ni wanawake wenye umri wa miaka 16 hadi 26, ambao wengi wakifika huko wanatumikishwa kwenye ukahaba katika nchi za India, Thailand, Indonesia na Malaysia.

Lugola alisema biashara hiyo inafanyika kwa usiri mkubwa na inafanywa na wanaofahamika akiwamo ndugu wa karibu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya kuzuia na kupambana na biashara hiyo, Adatus Magere, alisema wamefanikiwa kuokoa waathirika 147 huku 141 wakirejeshwa nchini na sita nje ya nchi ambao wameunganishwa na familia zao.

Alisema wanaendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya biashara hiyo, huku akielezea kamati hiyo inapita katika changamoto ya ukosefu wa fedha na vitendea kazi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Azzan Zungu, alisema Watanzania wasikubali watoto wao kwenda nje ya nchi kwa kuwa wengine wanatumikishwa hata kwenye matukio mabaya ya kigaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles