Upendo Mosha-Hai
DIWANI wa Kata ya Masama Mashariki, Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, John Munisi (38), amefikishwa mahakamani akidaiwa kumbaka na kumpa mimba mwanafunzi.
Munisi alifikishwa katika mahakama ya wilaya hiyo jana na kusomewa mashtaka mawili ya kubaka na kumpa mimba mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Marire mwenye miaka 17.
Akimsomea mashtaka mbele ya Hakimu Devotha Msofe, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Lubulu Mbise, alidai kuwa mshtakiwa ambaye ni diwani kupitia Chadema, alitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti.
Mbise alidai kuwa alitenda kosa la kwanza katika Kijiji cha Ngira wilayani humo ambako alimbaka mwanafunzi huyo Aprili 4, kosa alilotenda akijua ni kinyume cha sheria.
Alidai kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa la ubakaji kinyume na kifungu 130(1)(2) na kifungu 131 cha sheria ya kanuni ya adhabu sura 16 ya sheria iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2000.
Mbise alidai kuwa mtuhumiwa alitenda kosa la pili katika kijiji hicho hicho kwa kumpa ujauzito mwanafunzi huyo Aprili kinyume na sheria ya elimu kifungu 60(A)(2) na (3) iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mara baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa alikana kuyatenda na Hakimu Msofe aliahirisha shauri hilo hadi Julai 29.
Mshtakiwa huyo yupo nje kwa dhamana baada ya kukidhi masharti ambayo yalikuwa ni kuwa na watu wawili kila mmoja kuwa na barua inayotambuliwa kutoka kwa Serikali za mtaa au mtendaji na bondi ya Sh milioni mbili.