23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Bashungwa amjia juu Msigwa

RAMADHAN HASSAN – DODOMA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashugwa amemjia juu Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa (Chadema) baada ya kudai korosho ya Tanzania imeoza.

Hayo yalijiri jana bungeni jijini hapa wakati Msigwa akichangia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2019.   

“Serikali imekuwa ikisema inamjali mtu mnyonge, kimsingi mtu mnyonge kwa Tanzania ni mkulima, kwa bahati mbaya Serikali imewaletea adha na kuwavuruga wakulima wa korosho, sasa mmeanza kuwavuruga wakulima wa pamba,” alisema.

Wakati Msigwa akiendelea kuchangia, Bashungwa alimkatisha kwa kutaka kumpa taarifa na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson alimruhusu.

Bashungwa alisema anayosema Msigwa si kweli na Serikali haijawavuruga wakulima wa zao la korosho na korosho ya Tanzania ipo vizuri na ina ubora wa hali ya juu.

“Serikali haijavuruga wakulima wa korosho na korosho yetu bado ni bora na tunataka kuiambia dunia kwamba korosho ya Tanzania ni bora.

“Wewe ndio unavuruga wakulima na sio Serikali, tutangulize uzalendo kwanza,” alisema Bashungwa.

Msigwa aliendelea kwa kudai taarifa ya Bashungwa haipokei na kwamba wamepeleka bei za kinyonyaji na uporaji kwa wakulima wa korosho.

“Taarifa yake siipokei, hizi ni bei za kinyonyaji, hizi korosho bora mkazichome tu kwani zinaoza na  zitaharibu soko la baadae, hizi zichomeni moto,” alisema.

Kutokana na maelezo hayo, Bashungwa alisimama tena kwa kutumia kanuni ya 63 (4) na alimtaka Msigwa kuthibitisha kauli yake kwamba korosho zimeoza.

“Amesema korosho ya wakulima wetu imeoza na mimi nimetoka huko, korosho ni bora, athibitishe kama imeoza kweli kama haijaoza  achukuliwe hatua,” alisema.

Akilitolea ufafanuzi hilo, Naibu Spika alisema; “Nadhani Msigwa hoja yake ilikuwa kwenye korosho ipo maghalani inunuliwe, mheshimiwa Msigwa nyoosha mchango wako vizuri.”

Baada ya maelezo hayo ya Naibu Spika, Msigwa alisema; “Ningeomba nieleweke, sisi ni wabunge, tupo kuwatetea wananchi, tupo hapa kuwasemea wananchi. Hizi kodi zinamfanya mkulima apunjwe, hizi zinamfanya mtu wa mwisho anayeumia ni mkulima.

“Kama kweli mnawajali wanyonge mngewakumbuka wakulima wa pamba, mngewakumbuka wakulima wa mahindi.

“Mmewavuruga sana, shughuli ya korosho imewashinda, mngetuambia tumeshindwa tuanze upya, sababu ya ubishi tusipokuwa waangalifu mbona hamkupeleka jeshi kwenye pamba sasa hivi si hainunuliwi? Tunataka taifa letu liende mbele.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles