24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Askari JWTZ kizimbani kwa kuomba rushwa ya Sh 700,000

AVELINE KITOMARY NA ERICK MUGISHA (DSJ) – DAR ES SALAAM

 ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 77341 Johanes Kubambi, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru) kwa shtaka la kuomba rushwa ya Sh 700,000.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, Wakili wa Takukuru, Vera Ndeoya, alidai kuwa katika ofisi za jeshi la akiba, Wilaya ya Kinondoni, mshtakiwa aliomba rushwa kwa Kelvin Fabian ili aweze kumpatia nafasi ya mafunzo ya jeshi.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo na Ndeoya alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo aliiomba mahakama kutaja tarehe nyingine.

Hata hivyo, Hakimu Kiliwa alisema dhamana ipo wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao sio wanajeshi wala polisi na wawe na barua zinazotambulika kisheria, watakaotoa bondi ya Sh milioni 1 kila mmoja.

Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi Juni 28 kwa ajilii ya kutimiza masharti ya dhamana.

Wakati huo huo, Takukuru imempandisha kizimbani mfanyabiashara wa Kariakoo, Husen Khimji (41) kwa shtaka la kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Takukuru, Lupyana Mwakatobe, aliiambia mahakama kuwa Januari 22 maeneo ya Pub ya Junction, Khimji kwa udanganyifu alijipatia kiasi cha Sh 300,000 kutoka kwa Fatuma Mshumbuzi akimdanganya kumsaidia kumuwekea dhamana katika Mahakama ya Kisutu.

Mshtakiwa alikana madai hayo na Wakili Mwakatobe alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.

Hakimu Joyce Mushi alisema dhamana kwa mshtakiwa iko wazi kwa kuwa na wadhamini wawili watakaokuwa na vitambulisho vya taifa watakaosaini bondi ya Sh 500,000.

Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa tena Julai 9.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles