Francis Godwin, Mbeya
Wadau wa mazingira wanaozunguka Hifadhi ya Taifa ya Kitulo wilayani Makete mkoani Njombe wameanza mkakati wa kuulinda mmea wa chikanda usitoweke.
Mmea huo unadaiwa kuongeza nguvu za kiume na unasaidia wagonjwa walioathirika na Virusi Vya Ukimwi (VVU),umedaiwa kuwa hatarini kutoweka kutokana na kuingiliwa na majangili.
Diwani wa Kata ya Kitulo, Abel Mahenge, amesema baadhi ya watu nchini na nchi jirani kama Zambia na Malawi, wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya ujangili ndani ya hifadhi hiyo wakiwinda mmea huo ambapo huchimba na kuondoka na kiazi chake wakiamini ni dawa.
Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Itundu Wilaya ya Makete, Eva Ngombe amesema kupitia kikao hicho cha pamoja cha ujirani mwema wao watakuwa chachu ya ufikishaji elimu kwa jamii juu ya uhifadhi na ulinzi wa hifadhi ya Kitulo na hata kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ujangili ndani ya hifadhi hiyo.
“Ili kuendelea kulinda hifadhi na mmea wa chikanda kuendelea kubaki salama bila kuvamiwa na majangili, tumejiwekea utaratibu wa kulinda Hifadhi ya Kitulo kwa ulinzi shirikishi dhidi ya ujangili na uvamizi wa aina yoyote ile,” amesema.