26 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Nishati jua chanzo kipya cha mwanga barabara za Dar es Salaam

Andrew Msechu

MATUMIZI ya Umeme Jua katika miji na majiji yanazidi kushika kasi, japokuwa kwa miji na majiji yameunganishwa kwa kiwango cha juu kwenye Gridi ya Taifa na kuwa na umeme wa uhakika.

Kwa mujibu wa Shirika la Umeme nchini (Tanesco) zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa Dar es Salaam wameunganishiwa umeme, ikiwamo taasisi za Serikali zinazosimamia huduma za jamii na miundombinu ya barabara.

Meneka wa Wakala wa Barabara (Tarura) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi George Tarimo anasema pamoja na kuwepo kwa uhakika wa umeme, gaharama za umeme katika kuendesha taa za barabarani imekuwa ikionekana kubwa hivyo kulazimika kutafuta njia mbadala.

Anasema njia pekee inayotumika kwa sasa ni kutumia taa za mwanga wa jua ambazo tayari zimefungwa katika maeneo mengi ya manispaa za Temeke, Kinondoni, Ilala na Ubungo, kwaajili ya kupunguza gharama hizo.

Anasema hiyo inaonekana kuwa nafuu kwa kuwa mara tu ukishanunua taa hizo tauari umemaliza jukumu la kwanza, hivyo inakuwa ni mali ya Tarura na hakuna gharama za uendeshaji.

“Hizi taa za barabarani zinazotumia mwangajua gharama yake ni pale tu unapozinunua. Ukishanunua tayari umeshamaliza, huhitaji gharama nyingine kuziendesha kama ilivyo kwa taa zinazotumia umeme wa gridi.

“Ni wazi kwamba kama utaingia gharama baada ya kuzinunua, basi gharama hizo itakuwa pale tu zile betri zinazohitaji kuhifadhi chaji zinapoanza ku[ungua nguvu, au kama imetokea ajali na kuharibu mlingoti wa taa,” anasema.

Anasema eneo jingine linalotumika ni katika taa za barabarani za kuongoza magari, ambalo pia limekuwa likipewa ahueni kwamatumizi ya taa zinazotumia mwanga jua katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam.

“Hizi taa za kuongoza magari pia zinakuwa na matyumizi makubwa ya umeme ila ukitumia mwanga jua unaepuka hizi gharama. Kwa hiyo kwa kiwango kikubwa tumekuwa tukielekeza matumizi kwenye kununua taa za mwangajua na tayari zimefungwa kwenye maeneo mengi,” anasema.

Anaeleza kuwa kupitia utaratibu huo wanapunguza matumizi makubwa ya Serikali kwenye matumizi ya nishati katika suala la kusimamia usalama barabarani, hivyo kiwango kikubwa ambacho kinhetumiwa kwa kununua umeme kinaweza kuelekezwa katika huduma nyingine muhimu.

Kwa mujibu wa ripoti ya Energy Access Situation (EAS) ya mwaka 2016 iliyoandaliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) asilimia 99.3 ya kaya za Mkoa wa Dar es Salaam zimeunganishiwa umeme wa gridi ikifuatiwa na mikoa ya Rukwa (asilimia 91.2) na Kilimanjaro (asilimia 88.0).

Kaya ambazo mikoa yake inashika nafasi za mwisho kuunganishiwa umeme wa gridi ni pamoja na Lindi (asilimia 24.5), Njombe (asilimia 36.6), Mtwara (asilimia 38.9) na Katavi (asilimia 41.1).  

Aidha, kaya za mikoa ambayo inatumia umemejua kwa zaidi ya asilimia 50 ni Dodoma, Ruvuma, Katavi, Mtwara, Njombe na Lindi.

Kaya za mikoa ya Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Kigoma, Arusha, Morogoro na Mbeya zinatumia umeme jua chini ya asilimia 20.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi anasema barabara za Mkoa wa Dar es Salaam ndizo zinazoongoza kwa kutumia umemejua.

Anasema ingawa mkoa huo umeunganishiwa umeme kwa zaidi ya asilimia 99, bado zipo kaya zinazotumia umemejua na pia Halmashauri mbalimbali za mkoa Dar es Salaam zinatumia umeme jua katika barabara zake kwa kuwa ni nishati endelevu na ya uhakika.

Anasema kuwa hadi sasa barabara za Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni ndizo zinazoongoza kwa kutumia nishati ya jua.

“Nishati hii imeanza kuingia mjini, hata Dar es Salaam, sasa hivi ufungaji wa taa za barabarani, zinazotumia umeme jua, umekuwa mkubwa.Halmashauri ya Kinondoni inaongoza, ambapo barabara zote zinazojengwa upya ndani ya manispaa hiyo zinatumia umeme jua,” anasema.

Anaeleza kuwa kwa sasa taa za kuongoza magari zinazotumia umeme jua zinatumika katika maeneo ya Bamaga, Sayansi, Mnazi Mmoja, Barabara ya Nyerere mpaka kuelekea kule Uwanja wa Ndege na Gongo la Mboto na Kijichi.

Matimbwi anasema uhakika wa upatikanaji wa umeme jua kama ilivyo katika kituo cha daladala cha Simu 2000 ni moja ya sababu inayoongeza hamasa ya matumizi ya nishati hiyo jadidifu nchini.

“Wakati wa usiku mwanga unatakiwa uwepo wa uhakika kwa ya sababu ya usalama. Ndiyo maana katika kituo hicho hawakutumia taa zinazotumia umeme wa Tanesco,” anasema.

Itakumbukwa kuwa vyombo vivyorushwa angani kufanya tafiti ndivyo chimbuko la umemejua kwani vinahitaji umeme.

Matimbwi anafafanua kuwa maendeleo ya teknolojia ya umemejua imeweza kufikisha umeme mahali ambapo umeme wa gridi hauwezi kufika kwa wakati.

“Hata wananchi wa mijini, majumbani mwao wamefunga mifumo ya akiba ya umemejua ili umeme wa gridi unapokatika wasikose angalau mwanga,” anasema.

Matatizo ya vifaa bandia

Katika matumizi ya umeme jua, kumekuwa na matatizo yanayozungumzwa kuhusu vifaa bandia ambayo yanatokana na kuibuka kwa kundi la wafanyabishara wasiokuwa waaminifu ambao wamekuwa wakiharibu sifa ya vifaa hivyo.

Kwa Tanzania, ambayo watumiaji wake wanafikia wastani wa asilimia mbili ikilinganishwa na watumiaji wa nishati nyingine, vifaa bandia vinaweza kuwa na athari kutokana na kupungua kwa muwamko na uaminifu wa watumiaji dhidi ya wauzaji.

Katika taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti ya Ipsos Machi mwaka jana, ilibainisha kuwa asilimia 72 ya vifaa vya umemejua vinavyouzwa kwa bei ya chini havina ubora unaotakiwa.

Taarifa hiyo iliyopewa jina la ‘Solar off grid Market Research in Tanzania 2018,’ inaainisha kuwepo kwaongezeko kubwa la wauzaji wa vifaa hivyo ambavyo huingizwa nchini kwa njia za panya na kusababisha mamlaka husika likiwamo Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au Tume ya Ushinda (FCC) kushindwa kuhakiki ubora wa vifaa hivyo.

Ofisa Ukaguzi na Upimaji wa Ubora wa Vifaa vya Umemejua kutoka TBS, Anicetus Ndunguru, anasema kuanzia mwaka 2015 hadi Disemba 2018 jumla ya betri na solar 3,972 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 298.9 zilikamatwa na kuharibiwa hapa nchini, wakati betri na solar 2,547 zilirudishwa zilikotoka.

Anasema katika kukabiliana na udanganyifu huo, piataa 1400 za umeme jua zenye thamani ya Sh milioni 10 ziliharibiwa

Taasisi ya Kuendeleza Nishati Asilia na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania (Tatedo) inasema kuwapo kwa tatizo la vifaa feki vya umemejua vinavyoingizwa nchini ni mojawapo ya chanzo kikubwa kinachorudisha nyuma jitihada za Serikali.

Mmoja wa watumiaji wa umemejua kuatika eneo la Magole jijini Dar es Salaam, Seif Mfinanga anasema vifaa bandia vya umemejua ni janga ambalo Serikali na taasisi zake inatakiwa kulidhibiti ili wananchi wasipate hasara.

“Kwa sababu vifaa hivi tunanunua kwa bei ghali, lakini unapokuja kutumia siku moja mbili, vinaharibika ni hasara kwetu watumiaji.Lakini pia inatukatisha tama hata kutumia umemejua,” anasema.

Aidha, Meneja Mauzo kutoka Kampuni ya Chloride Solar, Ahmed Abdalla, anasema baadhi ya bidhaa kutoka China zimetamalaki katika soko la vifaa vya umemejua nchini, na kwamba bidhaa hizo baadhi ni feki jambo linachangia kudumaza matumizi ya nishati hiyo nchini.

“Lakini kuna changamoto ya ujio wa wachina kwa sababu ni wajanja sana, wameleta vifaa ‘fake’ jambo ambalo linavuruga soko la solar nchini. Kwa hiyo mtu anaingia gharama kufunga solar alafu baada ya siku mbili tatu havifanyi kazi,” anasema.

Hata hivyo, Matwimbwa anasema Tarea imekuwa ikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa wakaguzi wa taasisi mbalimbali zinazohusika na udhibiti wa vifaa hivyo, ikiwamo TRA, TBS na taasisi nyingine za Serikali ili kutambua ubora wa bidhaa hizo za umemejua kabla ya kumfikia mtumiaji.

“Kwa upande wa watumiaji huwa tunawaelimisha kwa kupitia vyombo vya habari, makongamano na maonesho kama vile siku ya nishati jadidifu ambayo huadhimishwa kila mwaka na hufanyika mikoa mbalimbali hasa ile yenye matumizi makubwa ya umemejua,” anasema.

Ofisa Ukaguzi na Upimaji wa Ubora wa Vifaa vya Umemejua kutoka TBS, Anicetus Ndunguru anakaririwa na gazeti moja la kila wiki akisema shirika hilo hukagua ubora wa vifaa vya umemejua kwa namna mbalimbali ikiwamo kutumia kuna mfumo wa udhibiti wa ubora kutoka kwenye nchi zinazokoagizwa kabla ya kusafirishwa kuletwa nchini.

“Tunao mawakala hususani nchi za Asia na Ulaya ambao hukagua bidhaa hizo kama zina ubora na mwekezaji husika hupewa cheti cha ubora. Akija huku sisi tunadhibitisha kwa kupitia hizo nyaraka.

“Ila bidhaa nyingi zinazalishwa nje ya nchi, ikitokea nyingine zimepita kuja nchini bila kukaguliwa, tuna maabara maalumu ya kupima vifaa vya sola, ni maabara iliyokamilika kabisa.

“Kwenye bidhaa za sola, kuna taa, betri, panel, inverter, chaja controller na vifaa vingine, vyote hivi maabara yetu ambayo ilianza tangu mwaka 2017 inapima ubora wake,” anasema.

Aidha, anaongeza kuwa iwapo mzigo wa vifaa hivyo ukihakikiwa na kubainika kuwa vifaa havina ubora unaotakikana, huharibwa nchini au kusafirishwa kurudishwa kwenye nchi ulikotokea kwa gharama za mwagizaji.

“Na wale walioingiza kwa njia zisizorasmi huwa tunafanya ukaguzi kwenye maduka na wasambazaji mbalimbali na hata kununua ili kupima ubora wake.

“Kwa ujumla udhibiti wa bidhaa za sola unaimarika, na wafanyabiashara hukimbia kutokana na hasara kwa maana mtu akiharibiwa mara moja hataki kukutana na kadhia hiyo tena,” anasema.

Upatikanaji wa umeme

Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme, katika nchi za Afrika Mashariki(EAC), Tanzania inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu wasiokuwa na umeme, kwamba watu milioni 36 sawa na asilimia 71 ya idadi ya watu nchini hawajafikiwa na umeme, Burundi ni watu milioni 10 sawa na asilimia 93 ya idadi ya watu nchini humo.

Aidha, kwa nchi za EAC, Kenya inaongoza kwa kuwa na asilimia kubwa ya watu waliofikiwa na umeme, kwa mujibu wa ripoti hiyo miaka miwili iliyopita watu waliokuwa na umeme Kenya ni asilimia 56, Tanzania asilimia 32.8, Rwanda asilimia 29.37, Uganda asilimia 26.7 na Burundi asilimia 7.5.

Kwa mantiki hiyo, kuendelea kuharibiwa kwa soko la vifaa vya umemejua ni mojawapo ya chanzo kinachoendelea kuzorotesha upatikanaji wa umeme nchini hasa vijijini. Kiujumla asilimia 87 ya watu duniani wasiofikiwa na umeme wanaishi maeneo ya vijijini.

Ripoti hiyo ya benki ya dunia inaonesha watu bilioni moja duniani au asilimia 13 ya watu duniani wanaishi bila umeme. Kwa nchi za Jangwa la Sahara, Afrika ya Kati na kusini mwa Asia ndiko kunkoongoza kwa kutokuwa na umeme.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni moja ya nchi zilizoonesha jitihada za kuwaunganishia wananchi wake umeme, nyingine ni Bangladesh, Ethiopia, Kenya ikifuatiwa na Tanzania ambazo zote zinaongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kwa asilimia tatu  kila mwaka kuanzia mwaka 2010 hadi 2016.

Lakini katika kipindi kama hicho, India ndio nchi iliyoongoza duniani kwafikishia umeme watu wake kwani zaidi ya watu milioni 30 kwa mwaka waliunganishiwa umeme.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles