24.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Mama mbaroni kwa kuchinja mwanae, kumpika

Na Harrieth Mandari , Geita

MWANAMKE mkazi  wa Kijiji cha Buligi, Kata ya Senga, Wilaya ya Geita mkoani hapa, Happyness Shadrack (36),  amedaiwa kufanya tukio la kinyama la kumuua kwa kumchinja mtoto wake wa kuzaa, Martha Yakobo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi sita na kisha kumkatakata vipande na kumpika.

Tukio hilo limetokea Juni 21, mwaka huu saa nane mchana.

 Inadaiwa Happyness akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi, Ruth Shadrack, alimchukua mtoto huyo aliyekuwa amelala kitandani na kumkatakata vipande vidogo vidogo na kisha kumweka ndani ya sufuria.

Kwamba baada ya kumkatakata mtoto huyo, aliwasha jiko na kuweka sufuria kisha kuanza kupika kama kitoweo.

Mtoto wa pili wa mwanamke huyo, Doris Yakobo, alisema alimuona mama yake akiwa anaweka sufuria jikoni na kuendelea kuchochea moto  lakini alipomuuliza alimjibu kuwa anachemsha maji na alipotaka kufunua kuangalia alimkataza.

“Mimi ndiyo nilikuwa mara nyingi nakaa na kumwangalia mtoto (marehemu), na siku hiyo baada ya mtoto kusinzia nilimpeleka chumbani nikamlaza kitandani, mama naye alikuwa kwenye chumba hicho hicho akiwa amelala,” alisema Doris.

Alisema baada ya kumlaza alitoka nje kwenda kulinda karanga  za bibi yake ili zisiibwe na kumwacha mama yake akiwa na mdogo wake wamelala.

Doris alisema baada ya muda alimuona mama yake akitoka na kuanza kuwasha moto, huku mkononi akiwa na sufuria iliyofunikwa ambayo aliinjika jikoni na kuanza mapishi.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Buligi, Manyoni Manyoni (CCM), alisema kuwa alipata taarifa za mauaji hayo akiwa kwenye kikao ofisini kwake.

Manyoni alisema alifika mwendesha bodaboda ofisini hapo na kumtafuta askari ambaye naye alikuwa katika kikao hicho.

Alisema mwendesha bodaboda huyo, alitoa taarifa kwa askari huyo kwamba kuna tukio la mama kumchinja mtoto wake.

“Baada ya taarifa hiyo, wote tuliokuwa kikaoni tulipatwa na mshtuko na tulilazimika kusimama na kwenda kwenye eneo la tukio ambako tulikuta unyama huo wa mauaji ya mtoto huyo umeshafanyika na mwanamke huyo alikuwa ameshakamatwa na polisi kwa hatua zaidi za mahoajiano na uchunguzi wa tukio hilo,” alisema Manyoni.

Ndugu wa mwanamke huyo, Amoni Mtani, alisema Happyness, amewahi kuathiriwa na ugonjwa wa malaria, hivyo anaamini kitendo hicho amekifanya kutokana na kutokuwa na akili ya kawaida.

“Ndugu yangu Happyness (mtuhumiwa) alishawahi kuugua malaria kali sana sasa hatujui labda imeathiri akili hadi kufikia kutenda kitendo hiki cha kinyama, unachinja mtoto na kisha kumpika jamani jamani tumuogope Mungu wetu,” alisema Amoni.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Dismas Kisusi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo pamoja na kushikiliwa kwa mtuhumiwa.

“Ni kweli tukio hili limetokea Juni 21 na tayari Jeshi la Polisi tunamshikilia mwanamke huyo kwa uchunguzi zaidi. Na uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mwanamke huyo ana historia ya kuwa na ugonjwa wa afya ya akili,” alisema Kamanda Kisusi

Alisema uchunguzi utakapokamilika jalada la mtuhumiwa huyo litapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aweze kulipitia kabla ya kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles