LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Derby, Frank Lampard wakati wowote kuanzia sasa anayetarajia kusaini mkataba wa kuinoa Chelsea, inaelezwa amemtaja mshambuliaji wa zamani klabuni hapo, Didier Drogba kutaka kufanya naye kazi katika benchi lake la ufundi.
Lampard anapewa nafasi hiyo kubwa ya kuchukua mikoba ya Maurizo Sarri anayetimkia Juventus, baada ya kukiongoza kikosi hicho msimu mmoja pekee na kufanikiwa kukiwezesha kutwaa ubingwa wa Ligi ya Europa.
Mchezaji huyo wa zamani klabuni hapo, amebakiza mkataba wa mwaka mmoja pekee na waajiri wake wa sasa Derby, ambao wanahitaji kiasi cha Pauni milioni nne kumuachia.
Hata hivyo, kabla ya kusaini mkataba wa kuinoa The Blues, Lampard anahitaji kuwasilina nawatu wake wa benchi la ufundi, miongoni mwao ni mchezaji mwenzake wa zamani, Didier Drogba.
Hatua hiyo inatokana na Drogba kuwa chachu katika mafanikio ya Chelsea aliyoichezea kwa miaka nane na kufanikiwa kufunga mabao 157, ambapo uwepo wake utakuwa na msaada mkubwa hasa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
Mbali na Drogba, lakini pia Lampard ataongozana na msadizi wake, Jody Morri ambaye pia aliwahi kuichezea Chelsea kuanzia mwaka 1996 hadi 2003, kabla ya kupewa majukumu ya kuinoa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 16.
Lakini wengine katika jopo hilo la benchi la ufundi, Lampard amemjumisha kipa wa zamani wa Manchester City, Shay Given, huku akiwaweka pembeni kina John Terry na msaidizi wa sasa wa Sarri, Gianfrnaco Zola.