27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA NEEMA Rostam kumwaga Mil 200, aahidi kusaidia zaidi GSM wapandwa mzuka, waitwanga Mil 300

NA MOHAMED KASSARA

-DAR ES SALAAM

NEEMA imefunguliwa, ndivyo unaweza kusema, baada ya klabu ya Yanga  jana kufanya harambee yake iliyopewa jina la ‘Kubwa Kuliko’ kwa mafanikio makubwa, kutokana na kukusanya mamilioni ya fedha taslimu na pamoja na ahadi kutoka kwa wadau mbalimbali wa michezo.

Harambee hiyo ilifanyika jana katika Ukumbi wa  Diamond  Jubilee jijini  Dar  Salaam.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alisema huo ni mwanzo mzuri wa klabu ya Yanga katika kutafuta mfumo mzuri wa uendeshaji wake kama ilivyo kwa wapinzani wao Simba, ambao tayari wamehama kutoka ule wa kadi za uanachama na kuwa umiliki wa hisa.

Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi wa tukio hilo, aliichangia Sh milioni 10 na kuwataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo pia kujitokeza kuisaidia.

“ Kwa ajili ya Yanga nitachangia Sh Millioni 10  na Katibu Tawala wa Morogoro ameniagiza niwaambie atachangia Sh laki moja.

“Wakati nakuja hapa, Rostam( Aziz)alinipigia simu na kuniambia  niwaambie atawachangia Sh milioni 200,  ataziwasikilisha kwa uongozi mara atakaporejea nchini kutoka Maarekani,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Katika hafla hiyo, zilichangwa zaidi ya Sh milioni 650, ambapo Kampuni ya GSM, iliahidi kutoa Sh milioni 300, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete Sh milioni tano, Kamati ya Hamasa Sh milioni 50, Kamati ya Utendaji Sh milioni 50 na wabunge mashabiki wa Yanga Sh milioni 40.

Mbunge wa CCM, Mariamu Ditopile Sh milioni moja, Mbunge Afrika Mashariki Sh milioni  1.4, wanawake mashabiki Yanga, Sh milioni moja huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiahidi kuipa Yanga ardhi eneo la Kigamboni.

Mkali wa mabao Uganda rasmi Yanga

Katika hafla hiyo, Yanga ilimtatangaza kumsajili mshambuliaji Juma Balinya kutoka Polisi ya Uganda.

Balinya, ndiye kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Uganda iliyomalizika hivi karibuni, akifunga mabao 19.

Awaki mshambuliaji alihusishwa na Simba , kabla ya jana  Yanga kumtambulisha kuwa mchezaji wao mpya.

Pia klabu hiyo ilimtambulisha kiungo Abdurlazizi Makame, baada ya  kumsajili kutoka Mafunzo ya Zanzibar.

Wachezaji wengine ambao wame mwaga wino  Jangwani licha ya  jana kutotambulishwa nini mshambualiaji, Maybin Kalengo kutoka Zambia, Sadney Urikhob (Namibia) na Patrick Shibomana kutoka Rwanda.

Wengine ni beki raia wa  Ghana Lamine Moro , Issa Bigirimana na Seleman Moustafa,  wote kutoka Burundi.

Kikwete atema cheche 

Akizungumza katika harambee  hiyo, Rais Mstaafu Kikwete aliutaka uongozi wa klabu hiyo, chini ya Mwenyekiti Mshindo Msolla kuwekeza katika soka la vijana ili kupunguza gharama za kufanya usajili wa wachezaji wa kigeni.

Kikwete ambaye alikuwa mgeni maalumu katika hafla hiyo, alitumia sehemu kubwa hotuba yake kuwaasa viongozi wenye dhamana katika michezo kutotumia madaraka yao kukandamiza timu ambazo hawazishabikii

“Kuna wakati Prof, Sarungi (Philemon)  alikuwa Waziri wa Michezo, Juma Kapuya alikuwa Waziri wa Michezo, wote ni Simba kinda kindaki lakini hawakutumia nafasi zaom  kukandamiza wengine(timu pinzani),” alisema.

Kikwete  alimtaka Waziri Mkuu Majaliwa kutoa mchango hata kama si shabiki wa Yanga, lakini pia akimtuma kufikisha ujumbe kwa Rais, John Magufuli akimtaka na yeye atoe mchango kwa klabu hiyo.

Nchemba kushusha kifaa matata

Mwanachama mwandamizi wa klabu hiyo, Mwigulu Nchemba aliahidi kushusha kifaa cha nguvu wakati wowote, kama alivyofanya kwa Feisal Salumu (Fei toto).

Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba na Magharibi na Waziri wa Zamani wa Mambo ya Ndani, msimu uliopita aliipa Yanga Fei toto kama mchango wake kwa timu hiyo.

Fei toto alisaini kuijunga na Singida United, lakini baadae Nchemba ambaye pia Rais wa klabu hiyo alimtoa Yanga.

” Kama ilivyokuwa kwa Fei toto, nilimsajili kama sehemu ya mchango wangu kwa Yanga, mwaka huu litakuwepo jembe moja ambalo tayari tumeshamalizana, tutamtangaza siku atakapokuja kufanya kazi kama Fei toto. alisema  Nchemba.

Mama Karume awaonya viongozi

Mjumbe wa Baraza la Udhamini wa Yanga, Mama Fatma Karume aliwaasa viongozi wa vyama vya soka nchini kuacha kutafuta umaarufu kupitia soka, badala yake waweke mbele maendeleo ya mchezo huo.

Alisisitiza timu za mpira wa miguu lazima zitumike kuwaunganisha Watanzania na sio kutumika kuwagawa.

“Niwaombe viongozi wa vyama vya mpira waache kutafuta umaarufu, wala wasitufanye tukawa na uhasama, mimi nakumbuka Hayati Mzee, Karume aliwahi kuinunulia Yanga nyumba, lakini alifanya hivyo pia kwa Simba, viongozi wa sasa wajifunze kupitia hayo,” alisema Mama Karume.

Mwakyembe awagomea ‘ maproo’

Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe alisema hakubaliano na utaratibu wa sasa wa timu kutumia idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni  katika mchezo mmoja.


“Msimu ujao nataka kuona sheria zinabadilika hasa kwa wachezaji wa kigeni ambao watacheza, ukisajili wachezaji 100 wa kigeni hatuna tatizo ila watakaocheza uwanjani hawatazidi watano ama wanne, na hili nitalisimamia kwa ukaribu.

“Sheria zipo na hazifuatwi, hakutakuwa na ruhusa kwa timu ambayo haina timu ya vijana kushiriki Ligi Kuu Bara, tunataka tujenge timu bora ya Taifa, lazima uwekezaji uwe mkubwa,” alisema Mwakyembe.

Manara ataka wakongwe wathaminiwe

Mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Sunday Manara aliwataka viongozi wa klabu hiyo kuthamini mchango wa wachezaji wa zamani wa timu hiyo, kwa kuwapa nafasi angalau mbili kwenye Kamati ya Utendaji.

Alisema wachezaji wa zamani wa timu hiyo wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali, lakini uongozi na wanachama wamekuwa wagumu kuwasapoti.

“Wachezaji wa zamani hatuthaminiwi, wengi wetu tupo katika mazingira magumu, tunashindwa kumudu hata gharama za matibabu, lakini bado hatupati mchango wowote kutoka kwa klabu yetu tuliyoitumiikia kwa moyo mmoja.

“Tunataka tupewe heshima inayostahili, zitengwe nafasi mbili kwa ajili wa wachezaji wa zamani, ili tutoe mchango wetu wa mawazo, nafasi hizi zinatakiwa kutolewa kwa wale ambao walicheza Yanga kwa maisha yao yote, hii itasadia kuhamasisha hata vijana wanakuja nyuma ,”alisema Manara.

Harambee kwa ajili ya kuichangia klabu hiyo ilizinduliwa jijini Dodoma kabla ya kuhitimishwa jana.

  Mpango wa kuichangia klabu hiyo   ulianzishwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera ambaye aliwataka wanachama na mashabiki wa timu hiyo kuichangia kiasi cha Sh bilioni 1.5 ili zitumike kufanya  usajili wa msimu ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles