KINSHASA, DRC
MWILI wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani, Etienne Tshisekedi ambaye pia ni baba wa Rais Felix, ulitarajiwa kuwasili jana baada ya miaka miwili tangu afariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya familia, mwili huo utawasili kutoka Ubelgiji kwa ajili ya mazishi.
Kiongozi huyo alifariki dunia mjini Brussels Februari 2017, akiwa na umri wa miaka 84, lakini mwili wake ulibaki katika mji huo mkuu wa Ubelgiji kutokana na wasiwasi wa siasa kwa utawala wa Rais wa zamani wa taifa hili, Joseph Kabila.
Kulingana na taarifa ya nduguye Askofu Gerard Mulumba, mazishi yake yatafanyika katika Viwanja vya Mashahidi.
Askofu Mulumba alisema baada ya kuukaribisha mwili katika uwanja wa ndege utasafirishwa hadi katika uwanja huo kwa maombolezo.
Alisema tayari maandalizi katika uwanja huo ikiwemo ujenzi wa jukwaa umekamilika mbali na yale ya maofisa wa polisi ambao wataongoza gwaride kumpatia heshima za mwisho baba huyo wa upinzani DRC.
Alisema takribani marais watano wa bara la Afrika wamethibitisha kuhudhuria mazishi yake.
”Ni zaidi ya miaka miwili tangu tulipoanza kutumia kila njia kuusafirisha mwili wake,” alisema Askofu Mulumba. ”Na sasa kwa kuwa hali iko shwari tunashukuru,” aliongeza.
Akiwa mwanasiasa wa muda mrefu, Tshisekedi alikuwa katika upinzani kwa miongo kadhaa lakini hakufanikiwa kuiongoza nchi hii.
Akiwa mkosoaji mkubwa wa aliyekuwa dikteta Mobutu Sese Seko, alianzisha chama cha Union for Democracy and Special Progress (UDPS) mwaka 1982 baada ya kuachiliwa kutoka jela na mwaka 1997.
Baada ya Mobutu kung’olewa madarakani na kundi lililoongozwa na Laurent Kabila, Tshisekedi alianza kuwa mpinzani wa utawala mpya , msimamo aliokuwa nao hata baada ya mauaji ya Kabila mwaka 2001 huku mwanawe, Joseph akipanda katika hatamu za uongozi.
Baada ya kushindwa katika uchuguzi wa 2011 uliodaiwa kukumbwa na udanganyifu mkubwa , Tshisekedi alikataa kutambua utawala wa Kabila hadi kifo chake.