TEL AVIV, Israel
ISRAEL inalazimika kufanya uchaguzi mpya Septemba mwaka huu, baada ya wabunge kupitisha hoja ya kulivunja bunge kutokana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kushindwa kuunda serikali ya muungano.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya bunge la nchi hii, Knesset, juzi kupitisha kura 74 dhidi ya 45 za kuunga mkono hoja ya kuvunjwa kwake na kuitishwa uchaguzi utakaofanyika Septemba 17 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani, DW, Waziri Mkuu Netanyahu ambaye ameiongoza Israel kwa muongo mmoja, alionekana kujipatia muhula wa nne madarakani lakini alishindwa kuafikiana na washirika wake hususan juu ya muswada unaopendekeza ulinzi wake dhidi ya tuhuma za rushwa.
Idhaa hiyo ya Kiswahili ilieleza kuwa kuliko kuachia jukumu hilo la kuunda serikali kwenda kwa mmoja wa mahasimu wake, chama cha Likud cha Waziri Mkuu Netanyahu kiliona bora kuwasilisha hoja ya kuvunjwa bunge ufanyike uchaguzi mpya ambao unakuwa wa pili ndani ya mwaka huu.
Netanyahu alisema taifa hilo linalazimika kuingia katika uchaguzi ambao haukuhitajika lakini anaamini chama chake kitaibuka na ushindi.
“Tutafanya uchaguzi mapema na kampeni za wazi zitakazotupatia ushindi. Tutashinda! tutashinda na umma utashinda. Ni vigumu kuamini kwamba Avigdor Lieberman sasa yuko upande wa kushoto. Avigdor Lieberman yuko upande wa kushoto,” alisema kiongozi huyo.
Idhaa hiyo ilieleza pia kwamba endapo muda wa mwisho ungepita ambao ulikuwa ni usiku wa saa sita bila ya kura kupigwa, rais wa nchi hii angeamua kumteua mbunge yeyote, ambaye alionekana kuwa kiongozi wa upinzani Benny Gants fursa ya kuunda serikali ya muungano.