25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wagonjwa wa dengue wafikia 1,900

CHRISTINA GAULUHANGA Na AVELLINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema wagonjwa wa homa ya dengue wanazidi kuongezeka na hadi sasa wamefikia 1,901 huku Kata ya Ilala, Dar es Salaam ikiongoza kwakuwa na wagonjwa 235.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi, alisema tangu watoe taarifa katika kipindi cha siku tisa, wamepata wagonjwa wapya 674.

Profesa Kambi alisema ni vyema wananchi wakachukua tahadhari kwa sababu hawana uhakika kama mafuta ya nazi na majani ya mpapai yanatibu ugonjwa huo kama ambavyo wengi wanaaminishana kwa sasa.

Alisema wamekuwa na wastani wa wagonjwa 75 kwa kila siku ikiwa ni tofauti na Aprili ambapo kuliwa na wastani wa wagonjwa 32.

“Ongezeko hili linasababishwa na uelewa kuhusu ugonjwa huu kwa wananchi, sasa hivi wengi wenye dalili wanajitokeza kupima katika vituo vya afya na tunaendelea kufanya tathimini kama kweli mafuta ya nazi na majani ya mpapai yanatibu,” alisema Profesa Kambi.

Alisema tangu kuanza kwa ugonjwa huo Januari, jumla ya watu 1,901 wamethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa huo ama kati yao 1,809 wanatoka Dar es Salaam.

Profesa Kambi alisema 89 walitoka Tanga huku Singida,  Kilimanjaro na Pwani walitoka mmoja mmoja.

“Hakuna vifo vilivyotokea hadi sasa tangu tamko lilipotolewa Mei 10 mjini Dodoma,” alisema.

DALILI ZA UGONJWA

Profesa Kambi alizitaja dalili za dengue kuwa ni kupata vipele vidogovidogo, kuvilia damu kwenye ngozi na kutoka damu sehemu za fizi, ndomoni, puani, macho na kwenye njia ya haja kubwa.

Alisema hadi sasa Serikali inapima ugonjwa huo bure katika vituo mbalimbali vya afya katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Amana, Temeke, Mwananyamala, Sinza, Vijibweni, Mnazi Mmoja, Lugalo, Mbagala, FFU Ukonga  na vituo vya Bombo na Horohoro mkoani Tanga.

“Serikali imeagiza vipimo vingine vya kupima wagonjwa 30,000  ambavyo vitasambazwa Dar es Salaam na maeneo mengine,” alisema Profesa Kambi.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Dk. Yudas Ndungile, alisema hadi sasa vituo vya kupima ugonjwa huo kwa Dar es Salaam na Tanga vimeongezeka kutoka saba vya awali hadi kufikia 19.

Alisema alili za dengue huanza kujitokeza kati ya siku tatu hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya ugonjwa huo.

Dk. Ndungile alisema hadi sasa kuna kata 20 katika Mkoa wa Dar es Salaam ambazo zimeripotiwa kuwa na wagonjwa zaidi ya 25.

Alisema kata hizo zinaongozwa na Ilala ambayo ina wagonjwa 235,  Upanga 87, Kisutu 86, Mbezi 78, Tegeta 27 na nyinginezo.

Aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuua mazalia ya mbu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles