31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Lissu atajwa kesi ya Zitto

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

SHABANI Hamisi ambaye ni shahidi wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amedai kitendo cha Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi na hajawahi kukamatwa mtu kuhusiana na tukio hilo, kilimfanya aamini maneno ya mshtakiwa kuwa Kigoma Uvinza kuna watu waliuawa.

Shahidi huyo wa tatu alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka.

Alidai Oktoba 29 mwaka jana akiwa Manzese, aliangalia YouTube kupitia simu ya Abilahi, akaona kwenye Ayo TV, Zitto akizungumzia polisi kuua watu Uvinza na wengine waliokwenda kupata matibabu walifuatwa na kuuawa.

“Nilishtuka polisi kufuata watu hospitali na kuwaua, nilichukulia kwa uzito sababu matukio hayo ni mengi, Tundu Lissu alifanyiwa hivyo, hakuna mtu aliyekamatwa  wala hatua zilizochukuliwa.

“Alipoongea Zitto nikachukulia moja kwa moja polisi wanahusika, si watu wazuri kwa raia, polisi kazi yao kulinda watu na mali zao na usalama wa nchi.

“Tundu Lissu kapigwa risasi hatua hazijachukuliwa, niliona si kitu kizuri ni kama ugaidi, niliona polisi si watu wazuri, niliwachukia sana na gari la polisi lilipokuwa linapita watu walikuwa wakizomea,” alidai shahidi.

Akihojiwa na Wakili wa Utetezi, Peter Kibatala kuhusu watu waliokamatwa kwa kuzomea polisi, alidai hakuna aliyekamatwa.

Shahidi mwingine, Mashaka Duma alidai yeye ni shabiki mzuri wa Zitto, anampenda, anaposikia sauti yake anafurahi, anapomuona kwenye televisheni pia anafurahi.

Alidai kuwa aliwachukia polisi baada ya kusikia kwenye YouTube Zitto akisema waliua watu Kigoma Uvinza.

Alidai roho yake imetulia baada kutoa hisia zake mahakamani kwamba analichukia Jeshi la Polisi kwa kitendo wanachodaiwa kukifanya Uvinza.

Shahidi huyo aliangalia YouTube akiwa Kimara Korogwe, Dar es Salaam. Kesi itaendelea leo saa tatu aaubuhi.

Awali aliposomewa maelezo ya awali Zitto alikana kwamba Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya Chama cha ACT Wazalendo kwa nia ya kuleta chuki miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la Polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Zitto alikana maneno ambayo anadaiwa kuyasema kuwa; “watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali Kituo cha Afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua’.

Jamhuri inadai maneno hayo yalikuwa ni ya uchochezi, yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Mshtakiwa anadaiwa kutoa maneno kwamba; ‘lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuawa na Jeshi la Polisi, pamoja na kwamba Afande Sirro amekwenda kule, halijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi… kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi, kuna taratibu za kisheria za kuchukua na siyo kuwaua, wananchi wengi sana wamekufa’.

Inadaiwa Zitto katika mkutano huo huo alitoa waraka kwa umma ukiwa na maneno ya kichochezi kwa nia ya kuleta chuki kwa Watanzania dhidi ya polisi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles