32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 1, 2023

Contact us: [email protected]

Kizimbani kwa utapeli

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam imempandisha kizimbani Anwari Shahame (35), mkazi wa Tabata kwa mashtaka mawili ikiwemo kukutwa na nyaraka bandia.

Akisoma shtaka la kwanza mbele ya Hakimu Anifa Mwingira, Mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Matarasa Hamisi, alidai kati ya tarehe zisizojulikana Machi mwaka 2015, eneo la Magomeni Mikumi, Wilaya ya Kinondoni mshtakiwa alipewa gari yenye namba za usajili T. 514 CVT aina ya Toyota Harriet yenye thamani ya Sh milioni 30 mali ya Kachenje Sabdiel huku wakijidai kumsaidia kuliuza lakini alikwenda kinyume na makubaliano.

Katika shtaka la pili mtuhumiwa anadaiwa kuwa katika tarehe isiyojulikana Mei mwaka 2016 katika Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa na nyaraka bandia ya mauzo ya gari hilo ambayo ilikuwa inaonesha tarehe 17 Mei, 2016 kwa lengo la kuonesha kuwa aliuza gari hilo kwa Nuru Nassib huku akijua ni uongo.

Mtuhumiwa alikana kufanya kosa la kwanza huku alikiri kufanya kosa la pili. Upande wa Jamhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.

Hata hivyo, Hakimu Mwingira alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaotoa bondi ya Sh milioni 10 kwa kila mmoja.

Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa tena Mei 28, mwaka huu.

Wakati huo huo, mahakama imempandisha kizimbani Juma Salim (27) mkazi wa Goba kwa shtaka la ubakaji.

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Karoline Kiliwa, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Neema Moshi, alidai mnamo Aprili 21 eneo la Goba Kinzudi, Wilaya ya Kinondoni, alimwingilia kingono  mwanamke mwenye umri wa miaka 28 bila idhini yake.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo huku upande wa Jamhuri ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa tena.

Hakimu Kiliwa alisema dhamana iko wazi kwa mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria watakaotoa bondi ya Sh millioni 1 kwa kila mmoja.

Hata hivyo mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi kesi yake itakaposomwa tena Mei 28. mwaka huu.

Mwishooo

Wauguzi walia wajawazito kutumia dawa za kienyeji

Na MOHAMED HAMAD – KITETO

WAUGUZI 114 wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wameomba Serikali kulipa deni lao ambalo ni Sh 91,080,000 kwa ajili za kununulia sare toka mwaka 2012, huku wakisema wajawazito kutumia dawa za kienyeji ni changamoto nyingine kwao.

Walisema waraka wa utumishi wa umma kumb namba CB 128/271/01/110 wa tarehe 01.09.2008 unamtaka kila muuguzi kulipwa Sh 120,000 kila mwaka kwa ajili ya kununulia sare za kazini.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, muuguzi Prisila Kalama kutoka Hospitali ya Wilaya ya Kiteto alisema pamoja na kutowapa stahili hizo wauguzi wamekuwa na sare kulingana na maadili ya kazi.

“Baadhi ya wauguzi wamechakaza sare (uniform) na kuja nazo kazini kinyume cha maadili, hivyo ili kulinda maadili yetu tunaomba tupate fedha hizo ambazo ni kwa mujibu wa waraka wa utumishi wa mwaka 2008,” alisema.

Kalama alisema mbali na tatizo hilo pia baadhi ya watumishi wamekuwa hawalipwi posho ya kuitwa kazini hasa kitengo cha upasuaji, pamoja na madai mengine ambayo wamekuwa hawalipwi kwa wakati.

Alisema pia uelewa mdogo wa baadhi ya wanajamii wanaowazunguka kuhusu sheria na taratibu za hospitali na vituo vya afya umekuwa na changamoto kwao kuwatuhumu, na kuwapa kashfa, matusi, kudhalilishwa na wakati mwingine kupigwa.

Changamoto nyingine aliyosema ni kuongezeka kwa matumizi makubwa ya madawa ya kienyeji kwa wajawazito wakati wa uchungu hali inayofanya matokeo mabaya kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamim Kambona, akizungumza na wauguzi hao aliwahakikishia kuwa ifikapo Julai atahakikisha watumishi hao wanalipwa fedha zao.

“Tulikuwa na changamoto ya kifedha, kwa sasa niwahakikishie mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kiteto hapa kuwa nitawalipa hata kwa kutumia vyanzo vyangu vya ndani ya halmashauri, lengo ni kulinda maadili yenu ya kazi ili muweze kufanya majukumu vyema,” alisema.

Katika hatua hiyo, Kambona aliwahakikishia wauguzi hao kuwa ataboresha hospitali hiyo, kukamilisha uzio, miundombinu ya maji kwa kisima alichochimba huku akidai atamkabidhi gari Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Dk. Pascal Mbota. 

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Mhandisi Tumaini Magesa aliwataka wanasiasa kuacha tabia za kwenda kutisha wauguzi na kudai hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika.

“Mwanasiasa na utaalamu wapi na wapi, iwe mwisho. Hata hivyo wauguzi toeni taarifa kwa wakati ili Serikali tuweze kushughulika na mambo hayo kwani haiwezekani kuvurugwa kwa mtindo huu wakati sisi tupo,” alisema Magesa.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Dk. Mbota, alisema kumekuwepo na jitihada kubwa zinazofanywa na watumishi wa idara ya afya ambazo zinatakiwa kutambuliwa pamoja na kwamba wanakabiliana na changamoto hizo.

“Natambua Serikali inataka tuwajibike kikamilifu kwa wananchi kama tufanyavyo siku zote ila mambo ya kisheria na kisera, nampongeza mkurugenzi mtendaji Tamimu Kambona kunipatia gari kwa ajili ya matumizi ya ofisi, itarahisisha kazi zangu,” alisema.  

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,400FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles