30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Watahiniwa kidato cha sita kuanza mitihani leo

LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta), limetangaza kuanza kwa mtihani wa Taifa wa kidato cha sita na ile ya kozi ya ualimu kwa ngazi ya stashahada na astashahada inayotarajia kuanza leo kote nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), Dk. Charles Msonde, alisema mitihani hiyo itaanza  leo na kufikia tamati Mei 23, mwaka huu.

Kuhusu mitihani ya kidato cha sita, Dk. Msonde alisema itahusisha watahiniwa 91,442, wakiwamo 80,305 wa shule na 11,117 wa kujitegemea.

Alisema kati ya watahiniwa hao 80,305 wa shule waliosajiliwa, wanaume ni 46,224 sawa na asilimia 57.56 na wanawake ni 34,081 sawa na asilimia 42.44.

“Aidha, watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 102, kati yao 67 ni wenye uono hafifu, 16 ni wasioona, 18 wenye ulemavu wa kusikia na mmoja ni mwenye ulemavu wa akili.

“Mwaka 2018 idadi ya watahiniwa wa shule waliosajiliwa walikuwa 77,222, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 3,083 sawa na asilimia nne kwa mwaka 2019 ukilinganisha na mwaka 2018,” alisema Dk. Msonde.

Kati ya watahiniwa wa kujitegemea 11,117 waliosajiliwa, wanaume ni 7,190 sawa na asilimia 64.68 na wanawake wakiwa ni 3,927 sawa na asilimia 35.32, huku watahiniwa wenye uoni hafifu wakiwa ni 15 na kwamba mwaka jana watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 10,421.

Kuhusu maandalizi ya mtihani huo, Dk. Msonde alisema tayari yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mitihani husika, vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani hiyo katika mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani.

Kuhusu mtihani wa kozi ya ualimu, alidai kuwa utahusisha jumla ya watahiniwa 12,540, wakiwamo 7,594  wa stashahada na 4,946 ni wa ngazi ya cheti.

Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa hao 7,594 wa stashahada waliosajiliwa, 5,615 sawa na asilimia 74 ni wanaume huku wanawake wakiwa ni 1979 sawa na asilimia 26.

Aidha, kati ya watahiniwa 4,946 wa ngazi ya cheti waliosajiliwa kufanya mtihani huo, 2,795 sawa na aslimia 57 ni wanaume na 2,151 sawa na asilimia 43 ni wanawake.

“Mwaka 2018 idadi ya watahiniwa wa ngazi ya ualimu waliosajiliwa walikuwa 7,422, hivyo kuna ongezeko la jumla ya watahiniwa 5,118 sawa na asilimia 41 kwa mwaka 2019 ukilinganisha na mwaka 2018,” alisema.

Alisema mitihani hiyo ni muhimu kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla kwa kuwa hupima maarifa, stadi na umahiri wa wanafunzi katika yale waliojifunza kwa kipindi cha miaka miwili cha elimu ya sekondari ya juu.

“Aidha, matokeo ya mtihani huu hutumika katika uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu pamoja na vyuo vya kati kusoma fani mbalimbali za utaalamu wa kazi kama vile afya, kilimo, ualimu, ufundi, sheria na mengineyo.

“Hivyo, mtihani huu ni muhimu sana kwa wanafunzi, wazazi, jamii na Taifa kwa ujumla. Matokeo ya mtihani wa ualimu husaidia kupatikana  kwa walimu ambao hufundisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Baraza linapenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha kuwa taratibu zote za uendeshaji mitihani ya Taifa zinazingatiwa ipasavyo. Kamati zihakikishe kuwa mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu.

“Kamati zote zinaelekezwa pia kuhakikisha usalama wa vituo teule unaimarishwa na kwamba vituo vitumike kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza,” alisema Dk. Msonde.

Alizitaja baadhi ya haki hizo kuwa ni pamoja na mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu.

Nyingine ni kuwaongeza muda wa dakika 20 kwa saa kwa somo la hisabati (sawa na saa moja kwa kila mtihani unaofanyika kwa saa tatu) na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kama mwongozo wa baraza unavyoelekeza.

Dk. Msonde alisema baraza hilo halitasita kukifuta kituo chochote cha mitihani endapo litajiridhisha pasipo shaka yoyote kuwa uwapo wake unahatarisha usalama wa mitihani ya Taifa.

Pia aliitaka jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa katika kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika kwa amani na utulivu.

Aliwataka Watanzania kuheshimu maeneo yote ambayo shughuli za mitihani zinafanyika na kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote asiyehusika na mitihani na anayeingia kwenye maeneo ya shule na vituo vya mitihani katika kipindi chote cha mtihani.

Aliwataka wasimamizi wa mitihani, wamiliki wa shule, walimu na wananchi wote kutojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mitihani hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles