BENJAMIN MASESE
Wawekezaji 48 kati ya 160 waliokuwa wanafanyia shughuli zao za uchumi kwenye majengo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya za Nyamagana na Ilemela Mwanza wametimuliwa.
Habari zinasema wengine wamejisalimisha baada ya chama hicho kufanya uhakiki na kuwabaini baadhi yao walipata vyumba hivyo kwa njia zisizo halali.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Salum Kalli alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya kuhitimisha uhakiki huo.
Alisema walibaini baadhi ya wawekezaji hawakuwa na mikataba halali kutoka kwa uongozi wa chama hicho, hivyo ilibidi waondolewe.
Kalli alisema baadhi ya wawekezaji walikuwa wamepangishwa na watu ambao wana mikataba halali kutoka kwenye uongozi wa CCM jambo ambalo ni kinyume na kanuni za fedha na mali za chama na jumuiya kama inavyoelekeza katika toleo la 2018.
“Kama mnakumbuka Mwenyekiti wetu, Rais Dk. John Magufuli alisema ni lazima mali za CCM zijulikane, tujue thamani yake, tuwatambue wawekezaji wetu katika majengo yetu na mambo mengine, ndiyo maana kama mkoa hatua hiyo imeanza na tumebaini mambo mengi.
“Mfano katika jengo la CCM la mkoa yaani hapa tulipo kuna ghorofa tano na tunao wawekezaji wengi.
“Lakini baada ya kufanya uhakiki wapo ambao baadhi tumewakuta hawana sifa za kuendelea kubaki, tumewaondoa na wengine wamejisalimisha tufakanya mazungumzo na wamebaki ambako vyumba vinne vipo wazi likiwamo eneo la duka la jumla kwa matumizi ya benki.
“Katika kitenga uchumi chetu pale Uwanja wa CCM Kirumba baada ya kuhakiki kila chumba tumebaini zaidi ya vyumba 43 vilikuwa na mikataba inayovunja kanuni za fedha na mali za chama.
“Hivyo tumewaondoa na vipo wazi kwa watu wengine watakaofuata taratibu, hatukubaliana kuona chama kikiwa na vitenga uchumi vyake kisha wanufaike wachache,”alisema.
Kalli alisema wakati akikabidhiwa ofisi mwezi mmoja uliopita na mtangulizi wake katika nafasi ya ukatibu, Adam Ngallawa, CCM ilikuwa ikiwadai wawekezaji hao zaidi ya Sh milioni 133.
Alisema alilazimika kuitisha kikao cha mazungumzo ya urafiki na kuwapa elimu jambo lililoongeza kasi ya ulipaji.
Alisema ndani ya mwezi mmoja zimeweza kukusanywa Sh milioni 60 ambazo ni sehemu ya Sh milioni 133 ya madeni ya wawekezaji .
Kalli alisema imani yake ni kuhakikisha ndani ya miezi minne atakuwa amafanikiwa kukukusanya kiasi kilichobaki.