23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Mahakama kutembelea ulipookotwa mwili

Na Dixon Busagaga-Moshi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi imefanya uamuzi mdogo wa kwenda kutembelea eneo lililotajwa na shahidi wa 18, Jackson Kileo (23) katika shauri la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi Humphrey Makundi.

Eneo hilo ni lile la Mto Ghona uliopo katika mji wa Himo Wilaya ya Moshi Vijijini, ambalo limetajwa katika shauri hilo kuopolewa mwili wa binadamu uliokuwa ukielea juu ya maji baada ya kufariki dunia.

Mtu huyo ambaye hakufahamika kabla, alipelekwa Hosptali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi na baadae kuzikwa chini ya uangalizi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

HOJA UPANDE WA MASHTAKA

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Frimin Matogoro kutupilia mbali pingamizi la mawakili wa upande wa utetezi waliyowasilisha juu ya hoja za upande wa mashtaka katika shauri hilo, mojawapo ikiwa ni kuhairisha kwa muda kutoa ushahidi kwa shahidi wa 18 kupisha shahidi wa 19.

Hoja ya pili iliyowasilishwa mahakamani hapo ni ombi la upande wa mashtaka kuruhusu shahidi wa 18, Kileo (23) mkazi wa Kilema Pofu, Wilaya ya Moshi kwenda kuionesha mahakama maeneo aliyotaja wakati wa kutoa ushahidi wake, ikiwemo umbali aliokuwepo wakati akiona mwili wa binadamu ukielea katika Mto Ghona.

Upande wa mashtaka katika shauri hilo namba 48 la mwaka 2018 ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Joseph Pande uliieleza mahakama kuwa ipo haja ya shahidi huyo na shahidi mwingine wa 19 kuionesha mahakama maeneo hayo.

Pande aliieleza mahakama kuwa sababu za kuomba hairisho la shahidi wa 18 kuendelea kutoa ushahidi lilikuwa ni kuruhusu kuendelea ushahidi wa shahidi wa 19 ambaye ni Mkaguzi wa Polisi, Inspekta Tenga, ambaye pia maelezo ya ushahidi wake yatalazimu mahakama kufika katika eneo la tukio.

 “Tutaiomba mahakama hii shahidi huyu aweze kuonesha sehemu husika, lakini pia mahakama kufahamu mazingira  yaliyotajwa ni muhimu sana. Tuna shahidi mwingine ambaye pia kwa ‘nature’ ya ushahidi wake pia tungeiomba mahakama apate fursa ya kuonesha maeneo hayo hayo yanayohusiana na tukio hilo,” alieleza Pande.

 “Ni rai yetu kwamba tuhairishe ushahidi ili tupate fursa ya shahidi wetu wa 19, ili mahakama itakavyoenda sehemu ya tukio kwa shahidi wa 18 na 19 mahakama iwe imejionea mazingira hayo, tumsikilize shahidi wa 19 ili tutakapoenda eneo la tukio tusiisumbue mahakama kurudi tena,” aliongeza Pande.

HOJA UPANDE WA UTETEZI

Akiwasilisha hoja za kupinga ombi hilo, wakili wa upande wa utetezi anayemtetea mshtakiwa wa tatu katika shauri hilo, Patrick Paul, aliieleza mahakama kuwa hakukuwa na sababu ya kutofautiana katika eneo hilo la kutembelea eneo na kwamba utofauti utakuwepo pindi shahidi mwingine atakapofika kutoa ushahidi.

 “Kwanini shahidi huyu asimalize halafu mwingine afuate, upande wa mashtaka haujaeleza sheria na utaratibu  wa kutembelea, sisi tunapinga ombi hilo kwa kuwa halikuonyesha limeletwa kwa misingi ipi,” aliohoji wakili Paul.

 “Sababu iliyotolewa ni eti mahakama ikatembee na kujionea  mazingira ya eneo lililozungumziwa, ni kuipa mahakama  kazi ya kwenda kukusanya ushahidi  wa ziada, Ni maoni yetu  utaratibu wa kutembelea  haupaswi kufanyika  katika kesi hii  na hata kama ikatokea  basi  hautafanyika katika  hatua hii,” aliongeza wakili Paul.

Alieleza kufanya hivyo itaibadili mahakama  kuwa shahidi  na kwamba kutakuwa  hakuna sababu  mashahidi pamoja na michoro ya eneo la tukio kupelekwa na kwamba wanapinga ombi la kwenda kutembelea eneo hilo  katika hatua  hiyo ya kesi.

UAMUZI WA JAJI

Akitoa uamuzi huo mdogo, Jaji Mfawidhi Matogoro alieleza  kuwa upande wa mashtaka ulihitaji shahidi wa upande wao kwenda kuonesha maeneo ambayo ameyataja katika ushahidi wake na kwamba atafanya hivyo pindi shahidi wa 19 atakapotoa ushahidi wake lengo likiwa ni kupunguza gharama za mahakama kwenda mara mbili eneo la tukio.

 “Anaeenda kuonesha eneo hili ni shahidi wa upande wa mashtaka, jambo hili si baya na upande wa utetezi utakapoomba mahakama kwenda eneo la tukio, itafanya hivyo pale itakapoona inafaa,” alieleza Jaji Matogoro.

Alieleza kwamba upande wa mashtaka baada ya kufunga kesi hautakuwa na nafasi ya kuomba kwenda eneo la tukio huku akieleza kuwa mahakama imeamua kwenda kutembelea eneo la tukio ili kujiridhisha na ushahidi uliotolewa.

Jaji Matogoro alieleza kuwa hakuna sheria ambayo inatoa katazo la ombi la upande wa mashtaka na kwamba kufanya hivyo ni kuunyima fursa upande huo kwenda kuonesha maeneo hayo yaliyotajwa katika ushahidi.

 “Nakubali ombi la kusitisha kuendelea na utoaji wa ushahidi wa shahidi wa 18,” alieleza Jaji Matogoro.

KABLA YA UAMUZI

Mapema kabla ya kufikia katika uamuzi huo, shahidi wa 18, Kileo akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Omary Kibwana, aliieleza mahakama kuwa mnamo Novemba 10 mwaka 2017 majira ya saa 10  za jioni aliona mwili wa binadamu ukielea juu ya maji wakati akivuka Mto Ghona akielekea Himo.

 “Nilikuwa navuka Mto Ghona kuelekea Himo, nikaona kitu kinaelea  ndani ya maji, nikasogea kwa karibu nikagundua ni mwili wa binadamu ukielea juu ya maji. Mwili huo ulikuwa umelala kwa tumbo  na ulikuwa umevaa kawoshi, bukta na soksi,” alieleza Kileo.

Alieleza kuwa mwili huo ulikuwa wa jinsia ya kiume na kwamba aliamua kumwita balozi wa mtaa  aliyemtaja kwa jina la Kiara na baadae kumtumia ujumbe wa maneno kupitia simu ya mkononi mwenyekiti  wa mtaa  aliyemtaja kwa jina la Robert Lekule.

 “Baada ya hapo walikuja Jeshi la Polisi  wakishirikiana na wananchi ambao nakumbuka alikuwepo Poul Minja  na Mmasai  ambaye simfahamu kwa jina.

“Wakati huo  mimi  nilikuwa pembeni ya mto nawaangalia walivyokuwa wakiutoa ule mwili, waliuweka kwenye  machela  halafu wakapekeka kwenye gari ya polisi.

 “Mwili uliwekwa kwenye machela ukiwa umeangalia chini, mwili ule ulikuwa  umevimba na kwa kukadiria ulikuwa na urefu kama  futi 4 na nusu mpaka 5,” alieleza Kileo huku akijibu swali aliloulizwa kuwa yeye anaweza kuwa na urefu wa futi ngapi na kujibu futi 6.

Kileo ambaye anafanya kazi za kilimo na ufugaji, alieleza kuwa akiwa kwa mbali na eneo alipowekwa marehemu aliweza kuona  mwili huo ukishushwa chini ukiwa kwenye machela kabla ya kuingizwa kwenye gari ili kutoa nafasi kwa wananchi kufika kwa ajili ya utambuzi.

 “Majira ya saa moja kasoro jioni polisi ndio walifika kuchukua mwili huo. Polisi walisema mwili huo wanaupeleka katika Hospitali ya Mawenzi, kipindi hicho kilikuwa cha mvua za vuli,” alieleza shahidi huyo.

Alieleza kuwa eneo analoishi ni ng’ambo ya Kilema, eneo la tambarare na kwamba kuna njia inayopita eneo la mto, njia ambayo imekuwa ikitumiwa na  wananchi kila siku wakipita kuelekea Himo.

Aliongeza kuwa  eneo ulipokuwepo mwili huo  ni la pori na korongo na maji yamekuwa yakituama.

 “Gari ya polisi lilikuwa upande wa Himo. Polisi walikuja wakitokea upande wa korongo (Himo), mwili ulipandishwa ukiwa kwenye machela, upande wa Himo lililopo gari la polisi na kipindi cha mvua kunakuwa na maji mengi, maji yakiwa mengi tunazunguka.

 “Maji yakiwa machache tunapanda hivyo hivyo tu. Kwa kipindi hicho kwenye korongo  maji yalikuwa machache. Wakati mwili unakuja kuopolewa mimi nilikuwa hapo hapo mtoni. Ukishapanda korongo kuna nyumba zimejengwa siku za karibuni. Kwa kipindi hicho ukipanda tu korongo kulikuwa  nyumba hazijajengwa bado,” alieleza Kileo ndipo Wakili Mkuu wa Serikali akawasilisha ombi mbele ya mahakama la shahidi huyo kuionesha mahakama eneo hilo.

Shauri hilo linalovuta hisia kwa wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini linaendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi kwa hatua ya upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wao.

Upande wa Jamhuri katika shauri hilo unaaongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Joseph Pande, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdalah Chavula, Wakili wa Serikali, Omari Kibwana na Wakili wa Serikali, Lucy Kyusa.

Upande wa utetezi unawakilishwa na wakili wa kujitegemea, Elikunda Kipoko na Gwakisa Sambo wanayemtetea mshtakiwa wa pili, Edward Shayo, wakili wa kujitegemea David Shilatu anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Hamis Chacha na wakili wa kujitegemea Patrick Paul anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Laban Nabiswa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,712FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles