Na KHAMIS SHARIF-MJINI MAGHARIBI
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Riziki Pembe Juma, ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuandaa vikao na wadau wa elimu ya juu, hali ambayo itasaidia kutatua matatizo yaliyopo baina yao na wamiliki wa vyuo hivyo.
Agizo hilo alilitoa jana mjini Unguja alipokuwa akizungumza na ujumbe wa tume hiyo uliofika ofisini kwake Mazizini, ambapo alisema vikao vya pamoja vya mashauriano husaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali.
“Lazima tuwe na uthubutu wa kukutana kila baada ya muda kujadili hali, mwenendo na mwonekano wa uendeshaji wa taasisi hizi, nadhani itasaidia,” alisema Riziki.
Aliitaka TCU kupanga utaratibu maalumu juu ya taasisi zinazotaka kuanzisha vyuo nchini ili kusaidia katika kupata taaluma bora kwa wanavyuo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Idrisa Muslih Hija, aliipongeza TCU kwa kuendelea kuyapatia ufumbuzi matatizo mbalimbali ya vyuo, hali ambayo inasaidia kukua kwa kiwango cha elimu nchini Tanzania.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, alisema wataendeleza mikakati waliyoiweka ikiwemo kutovipa fursa vyuo vya juu kuanzisha fani zisizosajiliwa na sheria za TCU.
Wakati huo huo, Wazir Riziki alikutana na uongozi wa Jumuiya ya Wasomi Wanawake Afrika (FAWE).
Ujumbe huo ulifika ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kuelezea masuala ya utoaji wa elimu ya kilimo cha mwani kwa wanafunzi watakaomaliza kidato cha nne.