Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), umesema upo tayari kumsaidia kisheria aliyekuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi Madeke, Hosea Manga (10), mkazi wa Kijiji cha Madeke Kata ya Mfriga wilayani Njombe, anayedaiwa kupigwa na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu na mwalimu anayetajwa kwa jina la Focus Mbilinyi, miaka miwili iliyopita na kusababishiwa kuvunjika uti wa mgongo.
Tukio hilo ambalo limedaiwa kufanywa na mwalimu huyo ambaye kwa sasa inasemekana amehamishiwa Kata ya Mtwango, lilitokea Machi 21, mwaka 2017 wakati Hosea akiwa na umri wa miaka (8) ambapo mtuhumiwa huyo anadaiwa kumwadhibu viboko kumi baada ya kukosa hesabu.
Akizungumza na gazeti hili Mratibu wa THRDC ,Onesmo Olengurumwa, alisema mtandao huo huwa una utaratibu wa kuwasaidia watu wanaohitaji msaada wa kisheria kwa kufuata taratibu ambazo zimewekwa.
“Sisi tukipata taarifa kuhusu kesi kama hiyo tunatumia wanachama wetu ambao ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ambapo tutawatumia taarifa za namna ya tukio lilivyotokea ambazo tunakuwa tumezipata kutoka kwa wahusika na wao najua watakapoanzia na kwa tukio hili kuna watu maalumu ambao wanawasaidia watoto,” alisema Olengurumwa.
Alisema ili wahusika waweze kushughulikiwa tatizo lao wanapaswa kuwa na nyaraka zote za muhimu na taarifa kamili ya tukio zima ikiwezekana wanaweza wakatoa mawazo yao nini wanahitaji.
Kauli ya THRDC imekuja wakati ambao baba mzazi wa mtoto huyo, Hosea Manga, akidai kuwa pamoja na kuendelea kumtibia mtoto wake lakini anahitaji msaada zaidi ili haki itendeke kwa kuwa kesi ya Jinai namba 83 ya mwaka 2017 waliyoifungua ili kumshtaki mwalimu huyo katika Mahakama ya Mkoa wa Njombe ilifutwa.
Alisema kesi hiyo ilifutwa baada ya daktari aliyemtibu mtoto huyo mara ya mwisho katika Hospitali ya Muhimbili kushindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi licha ya kuitwa mara nane.
Gazeti hili pia bado linaendelea kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Ole Sendeka, ambaye aliahidi kulishughulikia suala hilo kwa kuwa alishapokea malalamiko hayo ofisini kwake.
Mbali na Ole Sendeka, Mwanasheria Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Wakili Helman Danda, alikiri kesi hiyo kufutwa kwa sababu Jamhuri ilishindwa kupeleka shahidi ambaye ni daktari wa mwisho aliyemtibia mtoto huyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
“Ni kweli nimefuatilia nimeona kesi ilifutwa na sababu ni upande wa ushahidi ambaye ni daktari wa Muhimbili kushindwa kuja kutoa ushahidi, kwa mazungumzo zaidi mtafute Mkuu wa Mkoa,” alikaririwa Mwanasheria huyo alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili mkoani Njombe.
Mwandishi wa gazeti hili alifika nyumbani kwa mtoto huyo aliyekuwa akisoma darasa la tatu Kijiji cha Madeke umbali wa kilomita 103 kutoka Njombe mjini mapema.
Akizungumza na gazeti hili mtoto huyo alisema tukio hilo lilitokea Machi 21 mwaka 2017 akiwa na umri wa miaka (8) ambapo alipigwa na mwalimu kwa sababu ya kukosa hesabu.
Alisema siku ya tukio akiwa darasani kwenye kipindi cha somo la hesabu lililokuwa likifundishwa na mwalimu aliyemtaja kwa jina la Focus Mbilinyi ambaye aliwataka kufanya majaribio, yeye na wenzake wawili walikosa hesabu zote 10.
“Ilikuwa asubuhi tukiwa darasani tunasoma somo la hesabu mwalimu alitupa hesabu 10 na akasema ukikosa utachapwa kulingana na hesabu ulizokosa, hivyo mimi nilikosa hesabu zote na kutakiwa kuchapwa fimbo 10, mwalimu wakati anatuchapa, tulikuwa watatu, alituning’iniza kichwa chini miguu juu katika moja ya dirisha la darasani ndipo nilipoangukia mgongo na kuhisi maumivu makali yaliyosababisha hadi leo natumia muda mwingi nikiwa hapa kitandani,” alisema Hosea.
Kwa sasa mtoto Hosea anatumia muda wake mwingi akiwa amelala kitandani kutokana na maumivu makali anayoyapata baada ya tukio hilo la kuumia mgongo lililosababisha kutokea kwa kidonda kikubwa sehemu ya chini unapoishia uti wa mgongo.
Zaidi wakati wote wa ugonjwa wa takribani miaka miwili, ameshindwa kuendelea na shule.