Na Dixon Busagaga -Moshi
UPANDE wa Jamhuri katika shauri la mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Scholastica iliyopo wilayani hapa, Humphrey Makundi, umetoa taarifa ya maandishi ya kusudio la kuongeza mashahidi wengine watano.
Mashahidi wanaotajwa kuongezwa ni askari wa kitengo cha upelelezi kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro, E 9022 Koplo Enock, Mkaguzi wa Polisi, Leons Mwamunyi, Askari Kitengo cha Upelelezi, G 5865 Koplo Abdon, F 3988 Koplo Kibwana na H 1469 John.
Kuongezeka kwa mashahidi hao kunafanya idadi ya waliotoa na watakaotoa ushahidi kufikia 32.
Hadi sasa ushahidi wa watu sita umetolewa wakiwamo daktari aliyehusika katika uchunguzi wa mwili wa marehemu, baba mzazi wa marehemu na askari aliyesafirisha sampuli ya kielelezo cha vinasaba (DNA).
Mapema wakati akitoa ushahidi katika shauri hilo mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, Filimin Matogoro, shahidi wa sita katika shauri hilo, H 3487 Shabani Matumla, aliieleza mahakama kuwa alikabidhiwa sampuli kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande anayeiwakilisha Jamhuri katika shauri hilo, Matumla alieleza kuwa mnamo Novemba 19, mwaka juzi alipokea maelekezo kutoka kwa Mkaguzi wa Polisi, Victor Shamalaza, akimtaka kujiandaa na safari ya Dar es Salaam.
“Saa 11 jioni nilipokea maelekezo kutoka kwa Inspekta Victor Shamazala akinitaka kujiandaa na safari ya Dar es Salaam kwa Mkemia Mkuu kwa ajili ya kupeleka Sampuli,” alidai.
Matumla ambaye majukumu yake ni kukusanya takwimu za kijinai za mkoa katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kilimanjaro, alidai kuwa Novemba 20, mwaka juzi, saa tatu asubuhi alikabidhiwa sampuli mbalimbalii zilizokuwa zimehifadhiwa katika kontena zikiwa na lakili.
“Vielelezo nilikabidhiwa na Inspekta Victor Shamazala, vilikuwa ni (A) meno na mfupa, (B) damu ya Joyce Makundi, (C) ute wa mate wa Joyce Makundi, (D) damu ya Jackson Makundi na (E) ni ute wa mate wa Jackson Makundi,” alieleza.
Matumla alidai kuwa sampuli hizo alikabidhiwa kwa ajili ya kupeleka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam huku akieleza vitu vingine alivyopewa kuwa ni barua kutoka ofisi ya RCO na baada ya kukabidhiwa alielekea Uwanja mdogo wa Ndege wa Kisongo uliopo Arusha kupanda ndege.
“Nilipanda ndege ya Shirika la Coast, tulipitia Zanzibar ndiyo tukaelekea Dar es Salaam na tulifika saa saba hadi nane mchana. Baada ya kutoka uwanja wa ndege wa Dar es Saalaam nilielekea ofisi ya Mkemia Mkuu, Polisi Makao Makuu,” alieleza Matumla.
Alipoulizwa sababu za kwenda Makao Makuu ya Polisi zilikuwa ni nini, Matumla alieleza kuwa lengo lilikuwa ni kuchukua barua iliyomruhusu kwenda kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupeleka sampuli hizo.
“Nilifanya vile kwa sababu linapofika suala la malipo kwa ajili ya vipimo, ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali inawasiliana na ofisi ya DCI kwa ajili ya malipo ya vipimo na isingeweza kuwasiliana na ofisi ya RCO,” alieleza Matumla.
Pia alieleza kuwa barua kutoka ofisi ya DCI aliipata Novemba 21, mwaka juzi saa nne asubuhi ndipo akaelekea kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kupeleka vielelezo hivyo.
“Nilifika mapokezi na kueleza kilichonipeleka, nikakabidhi barua ya DCI, barua ya RCO na kifurushi kilichobeba sampuli pamoja na fomu PF namba 180, kabla ya kuondoka niliambiwa nisubiri na baadaye aliitwa mtaalamu aliyetajwa kwa jina la Hadija.
“Mkemia alianza kufungua kifurushi na kukagua kimoja baada ya kingine kulingana na kilichoandikwa katika barua, aliniruhusu kuondoka na kunitaka kuacha namba yangu ya simu kwa ajili ya mrejesho wowote wa taarifa,” alieleza Matumla.
Baada ya maelezo hayo, Wakili Pande alitaka kufahamu Novemba 20, mwaka juzi vielelezo hivyo alivitunza wapi ndipo Matumla akaeleza kuwa alivitunza katika chumba maalumu chenye jokofu na alikabidhiwa funguo kwa ajili ya kudhibiti hali ya joto.
Pia alisema alifika ofisini hapo na kukabidhiwa majibu ya DNA ambayo sampuli zake alizipeleka awali na baadaye kuanza maandalizi ya kurejea Kilimanjaro Novemba 30, mwaka juzi na kwamba baada ya kupanda ndege na alipofika alikwenda moja kwa moja ofisi ya RCO kukabidhi taarifa hiyo.
Wakili Pande aliuliza Januaru 30, mwaka jana alipokea nini na Matumla alimjibu kwamba alipokea simu saba kutoka kwa askari upelelezi Hashim ambaye kwa wakati huo alikuwa ni mtunza vielelezo katika ofisi ya RCO.
“Simu nilizopokea, tatu zilikuwa aina ya Itel, mbili Tecno, mbili Samsung kwa ajili ya kuzipeleka Polisi Makao Makuu kitengo cha makosa ya kimtandao kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi.
“Nilianza safari ya kuelekea Dar es Salaam nikiwa na askari wenzangu kwa kutumia gari aina ya Toyota Vits ambayo sikumfahamu mmiliki, isipokuwa ilikuwa ikiendeshwa na askari Ramadhan, na simu saba zilikabidhiwa Kitengo cha Makosa ya Mtandao,” alieleza Matumla.