30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Rungwe ataka ruhusa mikutano ya hadhara, maandamano

LEONARD MANG’OHA NA MANENO SELANYIKA

-DAR ES SALAAM

MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe, ameitaka Serikali kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho ambao pamoja na mambo mengine ulikusudia kufanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya watakaokiongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

“Tunapeleka ujumbe serikalini kwamba watufungulie tufanye siasa, waache kuzuia zuia hivi vyama, siasa ndiyo maisha ya mwanadamu, binadamu anaishi kwa maneno sasa ukizuia wananchi wanakosa pa kusemea. 

“Wakiwa na dukuduku zao wangesemea pale, lakini sasa hawana pa kwenda kutolea hayo maneno, kwa hiyo ni ujumbe wangu ninaoutuma kwenu kwamba Serikali iweze kurekebisha haya mambo watu wafanye siasa kama ilivyokuwa hapo nyuma,” alisema Rungwe.

Kuhusu uchaguzi huo, alisema viongozi waliokuwapo wamejitahidi kukifikisha chama hapo kilipo na kwamba watarudi madarakani ikiwa watachaguliwa tena na wanachama.

“Kwa hiyo sisi kwa kusema kweli hatuna mengi, mimi ninawategemea wajumbe, nitagombea na wenzangu watagombea, itajulikana baada ya uchaguzi kwamba nani ameshinda na nani hakushinda,” alisema. 

Rungwe alisema ikiwa atachaguliwa ataendeleza mapambano na kuhakikisha demokrasia inapatikana ili wananchi wapate pa kutolea dukuduku zao kwa sababu wamebanwa kiasi cha kushindwa hata kufanya mikutano.

“Kama hivi hapa sisi tumekutana, polisi walitakiwa waje kutulinda kama wao wana taarifa zozote kuwa kuna watu wanataka kuleta fujo, sio kutuambia tuondoke. 

“Chama chochote kinachotaka kufanya siasa kilindwe, tukitaka kufanya siasa za barabarani tulindwe, tukitaka kufanya siasa za majukwaani tulindwe, lakini sio kutwambia acheni na wengine unawaambia waendelee na siasa. Hili lazima lirekebishwe, limekaa vibaya” alisema Rungwe.

Alishauri kufanyiwa kazi sera ya njaa inayonadiwa na chama hicho ili kuwezesha wananchi kupata chakula cha uhakika kabla ya kuwaambia mambo mengine ya kimaendeleo.

Rungwe alisema hata watoto wasipopata chakula hawawezi kuelewa kile wanachofundishwa shuleni, hivyo ni lazima kuhakikisha wananchi wanalima kilimo cha umwagiliaji na si cha kutegemea mvua za msimu.

Alisema pamoja na kujengwa kwa reli itakayokuwa ikisafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda, itapendeza ikisafirisha mazao ya chakula kwenda katika nchi hizo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Zanzibar, Mohammed Masoud Rashid, alisema kufanyika kwa uchaguzi huo ni kutekeleza matakwa ya sheria ya vyama vya siasa nchini, inayotaka vyama vya siasa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano.

“Ni matumaini yetu kwamba tutafanikiwa ili tukienda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa tuwe tumemaliza,” alisema Rashid.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles