KIONGOZI wa Kanisa la Katoliki Duniani, Papa Francis jana aliongoza misa katika makao makuu ya kanisa hilo kuashiria kuanza kwa wiki tatu za Mkutano wa Maaskofu wa Kikatoliki kuhusu mabadiliko ya mifumo ya maisha.
Mkutano huo, unatarajia kufichua tofauti kati ya viongozi dhabiti wa Kikatoliki, wale wanaopendelea utamaduni kwa upande mmoja na wengine wenye misimamo wastani wanaokubali mabadiliko ya sera yanayoendelea kanisani.
Miongoni mwa mabadiliko hayo ni ndoa za wapenzi wa jinsia moja, talaka au hata watoto waliozaliwa nje ya ndoa.
Wachambuzi wa mambo wanasema kanisa hilo huenda lisibadilishe mifumo yake kuhusu masuala ya kifamilia licha ya kuwapo shinikizo la mabadiliko.
Papa Francis amewaomba maaskofu wawe na moyo wa kupokea mabadiliko katika maisha ya waumini wa kanisa hilo.
Hatua hiyo inakuja huku hivi majuzi tu, kiongozi mmoja wa kidini alitimuliwa kazini baada ya kubainika kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja.
Kwa mujibu wa msemaji wa Vatican, Kryzsztov Olaf Charamsa ambaye anatoka Poland, hawezi tena kuhudumu katika ofisi ya Vatican inayotetea itikadi ya Kikatoliki.
Charamsa amekuwa akisema msimamo wa Kanisa hilo kuhusu jamii ya jinsia moja ni wa kizamani na kwamba linapaswa kutambua maingiliano ya jinsia moja, na si kuyalaani.