WASHINGTON, Marekani
WATAALAMU wa uchumi nchini hapa, wameonya kwamba kuendelea kufungwa kwa serikali kunaweza kuathiri ajira za watu zaidi ya 500,000 mwezi huu.
Kwa mujibu wa watalaamu hao, jambo hilo linaweza kuongeza wastani wa kukosa ajira kuwa juu ya asilimia 4.0 endapo mgogoro katia ya Rais Trump na Bunge hutatafutiwa ufumbuzi kabla ya Ijumaa wiki hii.
Mgogoro huo ulianza Desemba 22 mwaka jana, baada ya Rais Donald Trump kuliomba Bunge kumuidhinishia dola bilioni 5.7 kwa ajili ya ujenzi wa ukuta kati ya nchi hii na Mexico.
Juzi hali hiyo ilisababisha watumishi wa serikali wapatao 800,000 kukosa mishahara yao.
Idara ya kazi ambayo haijaathiriwa na mgogoro huo, inadai imeshafanya utafiti kwa waajiri na kaya na imebaini kuwapo tatizo la ajira na ukosefu wa malipo ndani ya wiki iliyopita pamoja na Desemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa utafiti wa idara hiyo, katika kipindi cha mwezi huu kuanzia Januari 6 hadi Januari 19 mwaka huu, wafanyakazi wengi wa Serikali wapatao 380,000 watakuwa wamepungua wakati wengine watakuwa wanafanya kazi bila malipo, labda kama serikali itafunguliwa wiki hii.
“Hivyo, ikiwa serikali itaendelea kufungwa hadi Januari 19 mwaka huu, wafanyakazi wa serikali hawatapokea mishahara kwa wakati katika wiki hii ya utafiti.
“Inamaanisha kwamba tunatarajia kupungua malipo kwa watumishi kuanzia 500,000 hadi 600,000, “alisema Omair Sharif, ambaye ni mwanauchumi mkuu nchini hapa anayefanya kazi katika Benki ya Societe Generale, New York.
Alisema hali hiyo inaweza kusababisha kushuka kwa ajira kila mwezi ikiwa ni mara ya kwanza tangu Septemba 2010 na hivyo kumaliza kipindi cha miezi 99 mfululizo wa upatikanaji wa ajira.
Mtaalam huyo alisema endapo Bunge litachukua hatua za haraka kuwalipa wafanyakazi kama ilivyokuwa Oktoba 2013 wakati serikali ilipofungwa, tatizo hilo linaweza likatoweka.