*OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI
TANGU kupita miaka 95 Uturuki haijAwahi kuzongwa katika mizozo mingi ya kijeshi kama ilivyo sasa. Rais wa nchi hiyo, Tayyip Erdogan, anaendesha vita huko Syria, Iraq na pia ndani ya nchi yake mwenyewe dhidi ya waasi wa Wakurdi wa Chama cha PKK.
Ile kauli mbiu ya mwasisi wa taifa la sasa la Uturuki, Mustafa Atatürk, Amani nyumbani, amani duniani haifanyi kazi tena chini ya Erdogan. Haisikiki katika eneo kunakozungumzwa lugha ya Kituruki. Mbiu hiyo inasikika zaidi sasa upande wa Magharibi.
Wazo kwamba Uturuki itaingizwa na kuwa mwanachama Umoja wa Ulaya linazidi kutoweka, lakini Erdogan anataka kuhakikisha kwamba nchi yake ina ushawishi zaidi wa kisiasa na wa kiuchumi katika Kusini Mashariki ya Ulaya. Si tu katika nchi zenye Waislamu wengi, kama vile Albania, Bosnia na Kosovo, lakini anataka kupeperusha bendera ya Uturuki hata katika nchi za Wakristo wengi, kama vile Masedonia, Serbia na Hungaria.
Hatujaikubali mipaka yetu kwa hiyari yetu, alisema Erdogan katika hotuba yake aliyoitoa miaka miwili iliyopita. Lazima tuweko kote kule walipokuweko wazee wetu zamani, alisema mkuu huyo wa Uturuki. Uturuki ya sasa ni ndogo sana: Hatutokuwa wafungwa ndani ya kilomita za mraba 780000.
Pia nchi jirani za Ugiriki na Kuprosi zinauhisi mbinyo kutokana na siasa ya kujipanua ya Uturuki. Wakati ndege za kijeshi za Uturuki karibu kila siku zinaruka juu ya anga ya visiwa ya Ugiriki katika Bahari ya Aegean, ikisisitiza juu ya haki yake kwa eneo hilo, Uturuki hiyo hiyo inaibisha Jamhuri ya Kisiwa cha Kuprosi kuwa na haki ya madai ya rasilimali zilizoko katika bahari hiyo. Erdogan alitangaza: Yeyote anayebisha, basi atapata kofi la Uturuki shavuni mwake. Si tu alitamka hayo, Erdogan alituma pia manuwari za nchi yake ziranderande katika mwambao wa Kuprosi.
Katika Mashariki ya Kati na Bahari ya Mediterenia Erdogan anaonesha nguvu za nchi yake. Katika eneo la Balkan mkuu huyo kwanza anatumia nguvu za upole: kama vile uwekezaji, misaada ya fedha, kuendeleza harakati za utamaduni na dini.
Katika nchi za Balkan Uturuki inagharimia kujenga shule, vyuo vikuu, mabweni ya wanafunzi na misikiti, inafungua mabenki, jumuiya za kibiashara na vituo vya utamaduni.
Huko Serbia Uturuki inajenga vinu vya umeme. Erdogan ameahidi kuongeza uwekezaji katika nchi hiyo kutoka dola bilioni 1.7 hadi bilioni 5. Mabadilishano ya kibiashara baina ya nchi mbili hizo yamepanda juu zaidi ya mara mbili tangu mwaka 2015.
Katika barabara kuu kutokea Uturuki hadi Serbia pembezoni zimejaa hoteli na mikahawa ya Kituruki kuwahudumia madereva wa malori wanakuja Ulaya Magharibi. Rais wa Serbia, Aleksander Vucic, wakati alipofanya ziara Ankara mwezi Mei, aliipongeza Uturuki kuwa ni dola muhimu na yenye nguvu kabisa katika eneo la Balkan.
Pia Erdogan anaangaliwa kwa jicho zuri na Waziri Mkuu wa Hungaria, Viktor Orban. Alisema: Mwenyezi Mungu ametuletea Rais wa Uturuki. Nchi zote mbili zinataka kuimarisha zaidi uhusiano baina yao.
Orban, ambaye anadharauliwa na watu wengi katika Umoja wa Ulaya, anaangaliwa kwa jicho zuri na Erdogan na anaonekana huko Uturuki kuwa ni mshirika muhimu.
Kwa miaka Erdogan amekuwa anaota juu ya Uturuki Mpya, taifa kubwa lenye mipaka yake ya zamani. Televisheni ya Taifa, TRT, pamoja na vyombo vingine vya habari vilivyo karibu na serikali kila wakati huonesha ramani ya nchi ambamo Syria, Israel, Lebanon na maeneo makubwa ya Balkan na Afrika Kaskazini yamo katika eneo la dola la Uturuki.
Rais Erdogan alijielezea mwenyewe kuwa ni mwanasiasa anayevutiwa na moyo wa Taifa la Kituruki. Jambo hilo alilidhihirisha pale mwezi Mei alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Sarayevo.
Hapo kabla nchi nyingi za Ulaya zilimkatalia mkuu huyo wa Uturuki kuingia katika nchi hizo ili kufanya kampeni ya uchaguzi wa urais wa nchi yake. Lakini wafuasi wake 15000 walisafiri kutoka Ulaya Magharibi hadi Sarayevo. Erdogan alitoa mwito na kuwauliza washabiki wake: Je, mko tayari kuionesha dunia yote nguvu ya Waturuki wa Ulaya?
Upanuzi wa Uturuki tangu Karne ya 17 umeziingiza Uturuki ya sasa pamoja na eneo la Anatolia la Mashariki ya Kati, sehemu kubwa ya Afrika Kaskazini na Balkan. Alipoutembelea Oktoba 2013 Mji wa Prizren huko Kasovo, mji wenye athari kubwa za Kituruki, Erdogan alisema Kosovo ni Uturuki na Uturuki ni Kosovo.
Kosovo ni mshirika mkubwa wa kibiashara wa Uturuki. Ushawishi mkubwa iliokuwa nao Uturuki katika Kosovo ulionekana mwisho wa mwezi Machi pale idara ya usalama ya Uturuki, ikishirikiana na makachero wa Kosovo, ilpowakamata mjini Pristina na kuwapeleka Uturuki watu sita wanaoshukiwa kuwa ni mahasimu wa Erdogan na ambao ni wa kutokea kundi la Fethullah Gülen.
Pia huko Masedonia Uturuki inafanikiwa. Kampuni za Kituruki zimewekeza karibu Euro bilioni 1.2 na Idara ya Uturuki ya shughuli za dini, Diyanet, inajenga misikiti na shule za dini kwa ajili ya Waislamu walio wachache katika nchi hiyo. Katu hatutawaacha peke yao ndugu zetu, aliahidi Erdogan mwezi Februari.
Ikitegemea kibali cha Bunge la Ugiriki, Masedonia karibu itaumaliza mzozo wa jina lake na Ugiriki. Kwa hivyo, nchi ndogo ya Masedonia itajifungulia njia ya kujiunga na Umoja wa Kujihami wa Magharibi, NATO.
Pia mpango wa Umoja wa Ulaya wa kuzichukua kwa pamoja nchi za Balkan kama wanachama wake utapiga hatua kubwa mbele kutokana na suluhisho lililopatikana kuhusu jina jipya la Masedonia.
Hapo kabla uzito uliwekwa katika kuuzuia ushawishi wa Urusi katika eneo la Balkan, lakini sasa mambo yanabadilika- wasiwasi uko pia kuhusu ushawishi unaozidi wa Uturuki katika eneo hilo. Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aliliambia Bunge la Ulaya mwezi Machi mwaka huu kwamba yeye hataki kuiona Balkan inaelekea kwa Urusi au inaelekea kwa Uturuki.
Lakini Erdogan anaonekana ameazimia kuitimiza ndoto yake: Kwa hakika, sisi tutaijenga Uturuki iliyo kubwa, alisema mwisho wa Machi baada ya kuutwaa Mji wa Afir ulioko Syria. „Ikiwa lazima, tutatoa maisha yetu kwa jambo hilo- Ikiwa ni lazima tutayatoa maisha ya watu kwa jambo hilo. Hayo si maneno ya kuyadharau katika dunia ya sasa iliyojaa migogoro.