WASHINGTON, MAREKANI
MAREKANI inaonekana kubadili msimamo kuhusu uondoaji wa askari wake nchini Syria baada ya Mshauri wa Usalama wa Taifa nchini humo, John Bolton kusema haitawaondoa.
Bolton amesema wanajeshi wa Marekani hawataondoka kaskazini mashariki mwa Syria hadi pale wanamgambo wajiitao Dola la Kiislamu (IS) watakapotokomezwa na wapiganaji wa Kikurdi wanaoungwa mkono na Marekani watakapopewa ulinzi.
Kauli hiyo ya Bolton inaashiria kusitishwa kwa muda kwa mpango wa kuondolewa ghafla kwa vikosi vya Marekani uliotangazwa mwezi uliopita.
Lakini wakati Bolton akisema hakuna ratiba ya utekelezwaji wa mpango huo, Rais Donald Trump aliisisitiza dhamira yake ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani, ijapokuwa alisema hawataondoka wote hadi pale IS litakaposhindwa kabisa.
Akizungumza nchini Israel, Bolton amesema Marekani itawaondoa wanajeshi baada ya kuwaangamiza IS na kufikia makubaliano na Uturuki kuwalinda wanamgambo wa Kikurdi ambao wamekuwa wakipigana pamoja na Wamarekani dhidi ya makundi ya itikadi kali.