26.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Chuo cha mafunzo ya ndoa chaeleza kiini cha migogoro

Na KHAMIS SHARIF – ZANZIBAR



IMEELEZWA hatua ya kuanzishwa kwa Chuo cha Maadili ya Ndoa Zanzibar kutasaidia kupunguza wimbi la utoaji talaka kiholela visiwani hapa.

Akizungumza jana mjini Unguja katika mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana wanaotarajia kuingia katika ndoa hivi karibuni, mkufunzi wa mafunzo hayo, Sheikh Iddi Said, alisema chuo hicho kinaweza kuwa msaada mkubwa wa kudumisha ndoa na kupunguza talaka katika jamii.

Alisema utafiti unaonesha chanzo cha ndoa nyingi kuvunjika ni kukosekana kwa elimu ya maadili ya ndoa kwa jamii, ambayo wakati mwengine huchangiwa na uwepo wa vijana kukurupuka kuingia katika ndoa bila kupata mafunzo ya ndoa.

Sheikh Said alisema chuo hicho kimelenga kutoa mafunzo maalumu ya kuwajenga wanandoa kuwa na mapenzi, huruma, uadilifu na maadili wakati wote wanapokuwa kwenye maisha yao ya ndoa.

“Hata hivyo pia viongozi wa dini ni lazima watambue kwamba wana wajibu katika kufungisha ndoa, toeni elimu ya ndoa kwani nyingi huvunjika na nyingine kutetereka, hii ni kukosekana kwa misingi haswa,” alisema Sheikh Said.

Akizungumzia kukithiri kwa vitendo viovu, Sheikh Said alisema matendo mengi yamechangiwa na kuporomoka kwa maadili kwa wanandoa ambao wengine husababisha hata watoto kukosa malezi bora.

Nao baadhi ya mashekh na makadhi walioshiriki mafunzo  hayo, walisema kwa miaka iliyopita hakukuwa na wimbi kubwa la kuvunjika ndoa kutokana na wazee wengi walikuwa wakifundisha maadili ya ndoa watoto wao na jinsi ya kuishi kwa mume na mke jambo ambalo lilisaidia kustawisha ndoa na familia kwa ujumla.

Sheikh Abdulhafuri alisema kupotea kwa maadili ya Kizanzibari kumechangia ndoa nyingi kuvunjika kutokana na kuiga maadili ya kigeni.

Naye Mkuu wa Chuo cha Maadili ya Ndoa Zanzibar, Sheikh Ali Abdallah Amour, alisema licha ya kufunguliwa kwa chuo hicho, lakini mwamko bado mdogo kwa jamii kujiunga.

Alisema hadi sasa ni wanandoa 94 ndio waliojitokeza na kujiunga na mafunzo hayo ambapo kati ya hao wanafunzi 30 waliweza kuhitimu mafunzo hayo na kutunukiwa vyeti vyao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles