25.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

SHIDA YA UZAZI INAYOWAKABILI WAJAWAZITO SIMIYU

Na VERONICA ROMWALD – ALIYEKUWA SIMIYU


“MKE wangu alipata ujauzito wa kwanza mwaka 1993, usafiri ulikuwa wa shida wakati huo. Nakumbuka jinsi alivyoteseka alipofikia kipindi cha kujifungua.

“Njia yake ya uzazi ilikuwa ndogo, lakini kwa kuwa katika Kituo cha Afya Nasa hapa Wilaya ya Busega huduma za uzazi hazikuwa bora, tulilazimika kusafiri hadi wilayani Magu,” anasimulia Makaranga Matomo.

Matomo ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Nyashimo wilayani humo, anasema safari ya kutoka Busega kwenda Magu ni ndefu hali iliyotishia uhai wa mke wake na mtoto.

“Jambo jingine lililotufanya kwenda Magu licha ya umbali uliopo kutoka Busega, ni changamoto ya uhaba wa dawa, vifaa tiba na watumishi wa kutosha katika Kituo cha Afya Nasa.

“Tulilazimika kutumia usafiri wa kawaida (daladala) kuweza kufika huko Magu, Pale kituoni tulisubiri gari kwa takribani nusu saa, ilipofika tulipanda na kuanza safari ya kuelekea hospitalini.

“Kama unavyojua tena daladala kwa kawaida huwa linakwenda na kusimama ili kushusha na kupakia abiria, hivyo njiani tulitumia dakika takribani 45 hadi kufika Magu.

“Tulifika salama lakini mke wangu alikuwa amechoka, alijifungua kwa taabu mno ilikuwa kidogo tu angepoteza maisha yake, mtoto au wote kwa pamoja,” anasimulia.

 

Kisa kingine

Mkazi wa Busega, Anna George (78) anasema kamwe hawezi kusahau siku aliposhuhudia mjamzito akipoteza maisha mbele ya macho yake wakati alipokuwa akisaidiwa kujifungua.

“Mama yule alikuwa ame;pelekwa hospitalini wakitokea kijiji cha mbali, walilazimika kutumia usafiri wa ng’ombe hadi kufika pale,” anasema.

“Wataalamu walimsaidia kujifungua lakini haikuwezekana kwa sababu tayari yeye na mwanae walikuwa wameshachoka hivyo, wote wawili walipoteza maisha,” anasimulia.

 

Uchungu hauvumiliki

Kwa kawaida mama anapohisi uchungu wa uzazi huwa hawezi kuuvumilia hivyo huhitaji msaada wa haraka ili aweze kujifungua salama.

“Uchungu ule huwa hauna ‘simile’ unapofika mama huhitaji kusukuma mtoto ili mtoto atoke, hawezi kujizuia kabisa, ni lazima ajifungue,” anasema Nyakato Jumanne.

Anasema katika kipindi cha miaka 10 iliyopita wajawazito mkoani humo walihangaika kupata huduma bora za uzazi tofauti na miaka ya sasa.

“Hospitali zipo mbali, usafiri nao ulikuwa wa shida. Nakumbuka siku moja nilimsaidia mjamzito kujifungua, alikuwa akitembea kwa miguu kuelekea hospitalini kujifungua.

“Alishindwa kufika. Ikanilazimu kumwelekeza namna ya kufanya kwa sababu ilikuwa ni mimba yake ya kwanza. Sikukumbuka hata kuvaa mipira, nikamsaidia kumpokea mtoto kwa sababu kichwa kilishaanza kutoka.

“Bahati nzuri alikuwa na vifaa, nikachukua wembe nikafunga vizuri kitovu na kukata panapotakiwa, nikamtoa mtoto, tukasubiri kidogo kondo la nyuma nalo likatoka wakaendelea na safari kuelekea hospitalini,” anasimulia.

 

Kujifungua mwenyewe kwahitaji ujasiri

Eliza Kanzi anasema wakati mwingine huhitaji ujasiri mjamzito kuweza kujifungua akiwa mwenyewe, na kwamba yeye ameshawahi kupitia hali hiyo.

“Ulikuwa ujauzito wangu wa sita, nilikuwa mwenyewe nyumbani nilipohisi kuumwa dalili za uchungu, mume wangu alikwenda kazini kutafuta riziki,” anasema.

Anasema aliangalia katika mkoba wake kama kuna vifaa vyote anavyohitajika kuwa navyo, akajiridhisha.

“Vilikuwa vimeenea, lakini sikuweza kutoka nje kwenda popote, uchungu ulizidi kukolea, ikabidi nivae ujasiri na kujisaidia mwenyewe kujifungua.

“Baada ya mtoto kutoka nilichukua wembe nikakata kitovu na kusubiri kondo litoke. Nikakaa kidogo nikapata nguvu, nikasimama na kuchungulia nje nikamuona mtoto mmoja alikuwa anacheza.

“Nikamuita na kumuomba kwenda kuniitia mama yake ambaye nilimweleza namna nilivyojifungua hivyo nahitaji msaada, akanisaidia na baadae nikapelekwa hospitalini,” anasimulia.

 

Mkunga wa jadi

“Suala la uzazi hapa Busega linawatesa wanawake, wengi walikuwa wanakuja kwangu niwasaidie,” anasema Bilimbe Isaya (54) ambaye ni mkunga wa jadi.

Anaongeza: “Nimeshuhudia vifo kadhaa vya uzazi, nikikumbuka huwa nasikitika, unakuta mama amefikia hatua ya kujifungua anasafirishwa katika kituo fulani cha afya lakini akifika pale huduma hakuna, anapewa rufaa kwenda kituo kingine.

“Umbali wa kutoka kituo kimoja kwenda kingine ni mrefu matokeo yake walikuwa wanajifungulia njiani na wengine walijifungua nje ya hospitali nikishuhudia,” anasimulia.

 

Mradi wa afya

Felister Bwana ni Meneja Mradi Afya ya Mama na Mtoto wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA- Tanzania), anasema hali hiyo iliwasukuma kushirikiana na serikali kuboresha huduma hasa za afya ya uzazi mkoani humo.

“UNFPA tunaamini lazima tuwe na dunia inayothamini mimba, kila uzazi ni salama na kila malengo ya kijana yanaweza kufikiwa,” anasema.

Anasema shirika hilo limejenga wodi mpya za wazazi katika vituo vya afya 12 kati ya 38 vilivyopo mkoani humo.

“Pamoja na ujenzi huo, pia tumewapa vifaa tiba vya kisasa vituo vyote 38 pamoja na magari tisa ambapo kati ya hayo matatu ni ya kubebea wagonjwa (ambulance) na sita ni kwa ajili ya uratibu wa shughuli za afya ya mama na mtoto,” anasema.

Anasema hayo yameweza kufanywa kupitia mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto mkoani humo uitwao ‘Nilinde, Nikulinde’ unaotekelezwa na UNFPA kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Watu wa Korea (KOICA).

“Ujenzi huu umesimamiwa kwa ukaribu na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Simiyu na Halmashauri zote sita za mkoa huu,” anasema.

Mwakilishi Mkazi wa UNFPA-Tanzania, Jaqueline Mahon, anasema wataendelea kushirikiana na serikali kuboresha huduma za afya hasa ya uzazi nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa KOICA-Tanzania, Kira Thomas anasema kupitia mradi huo jumla ya vituo 13 vimetenga maeneo maalumu kwa ajili ya kuhudumia vijana.

“Pia, wataalamu 70 wamepatiwa mafunzo maalumu ya kuwawezesha kutoa huduma rafiki kwa vijana, ni matarajio yangu kwamba vijana watajitokeza kwa wingi kujifunza kuhusu afya ya uzazi na hiyo itasaidia kukabili vifo vitokanavyo na uzazi kwani watajitambua,” anasema.

Anasema pamoja na hao, watoa huduma za afya 350 wamepatiwa mafunzo ya ngazi mbalimbali za namna ya kutoa huduma za dharura kwa kina mama wakati wa kujifungua.

“Aidha, jumla ya watoa huduma ngazi ya jamii 150 wamepatiwa mafunzo ya kutoa huduma salama, afya ya mama na mtoto na uzazi wa mpango katika jamii zinazowazunguka.

“Ni matumaini yangu wananchi wa Simiyu watanufaika kwa uwapo wa huduma bora za uzazi salama na hivyo kusaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na kina mama wakati wa kujifungua,” anasema.

 

RC Mtaka

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka anasema mkoa huo una vijiji 480, zahanati 190 na kwamba wanahitaji kuwa na vituo vya afya 140 kuweza kukidhi mahitaji.

“Matarajio yetu ni kwamba wadau wote wanaounga mkono serikali kwenye shughuli za afya wajielekeze kwenye ujenzi wa majengo zaidi kuliko semina,” anasema.

Anaongeza: “Haipendezi kwa mfano kuona mdau anatumia Sh bilioni tatu kujenga uwezo wa wataalamu wakati tunakabiliwa na uhaba wa majengo kwa kiwango cha asilimia 50.

“Hivyo, kwa hatua hii tunashukuru wadau wetu UNFPA na KOICA wametuelewa na kutuunga mkono katika suala hili,” anasema.

 

Kauli ya waziri

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo, anasema kuanzia sasa serikali haitapandisha hadhi tena kituo cha afya kuwa hospitali ya wilaya, badala yake itaendelea kujenga vituo vipya na kuweka vifaa vya kisasa vinavyohitajika.

“Kufanikisha lengo hilo katika mwaka huu wa fedha 2018/19 serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 105 zitakazotumika kujenga hospitali 67, tumedhamiria kufanya mabadiliko katika awamu hii.

“Ikumbukwe tangu enzi za Uhuru hadi kufikia mwaka 2005, alipochaguliwa  Rais John Magufuli, tulikuwa na vituo 515 pekee vya hospitali kati ya vituo 4,420. Aidha, kati ya vituo 515 vilivyokuwa na uwezo wa kutoa huduma ya dharura kwa wajawazito ni 115 tu nchi nzima.

“Lakini katika kipindi cha miaka miwili ya Rais Dk. Magufuli tumeweza kujenga vituo vipya 208 ambavyo vitatoa hadi huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito, na serikali imetenga Sh bilioni 38.9 kwa ajili ya kujenga vituo vingine 97,” anasema.

Anasema hatua hiyo itasaidia kukabili vifo vitokanavyo na uzazi kwani wajawazito watapewa huduma kwa wakati mwafaka pale itakapohitajika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles