27.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 26, 2022

INAWEZEKANA KUITAMBUA DAWA BANDIA KIRAHISI

KWA kawaida ugonjwa unapoingia mwilini, jambo la kwanza lilofanyika mara baada ya kufika hospitalini ni kupatiwa vipimo kisha dawa kwa ajili ya kuutibu.

Inafahamika kuwa lengo kuu la matumizi ya dawa pamoja na vifaa tiba ni kuzuia, kutibu, kusaidia kubaini magonjwa na kurekebisha mifumo ya mwili.

Yapo malengo yaliyofikiwa baada ya matumizi ya dawa pamoja na vifaa tiba, ambapo ni matokeo chanya katika huduma za kiafya.

Licha ya kwamba unapopata tiba lengo huwa ni kupata matokeo chanya, bado zipo changamoto zinazokwamisha juhudi za wataalamu katika kupambana na magonjwa, hatimaye kusababisha baadhi ya magonjwa kuendelea kuwapo na kuathiri jamii.

Ili kufikia malengo chanya ya utoaji wa huduma bora kwa wanajamii, bado kunahitajika uwapo wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi/bidhaa za maabara vilivyo na ubora unaotakiwa ili kuweza kutibu au kutokomeza ugonjwa husika katika kipindi sahihi.

Moja ya changamoto zinazoathiri huduma za afya ni uwapo wa dawa au bidhaa zisizo na ubora unaotakiwa, ili kumsaidia mgonjwa.

Dawa au bidhaa kutokuwa na ubora unaotakiwa hujumuisha upungufu katika kiwango cha chembechembe zilizomo ndani yake baada ya kutengenezwa. Upungufu mwengine unaweza kutambulika kwa kutazama kwa macho au njia za kitaalamu.

Kuna baadhi ya upungufu katika dawa unaweza kutambulika kwa kuzitazama kwa macho, mfano muundo wa vidonge, ndani ya kifungashio si kawaida kukuta vidonge au dawa ya aina moja kuwa na maumbile au rangi tofauti au hata saizi ya vidonge itofautiane katika ‘blister/strip’ moja. Kuna baadhi ya dawa huwa na harufu ya kipekee ambapo ukiifungua unaweza kubaini tofauti iliyopo endapo umewahi kuitumia au kuiona hapo kabla.

Unaweza kuangalia aina ya uandishi katika kopo au kifungashio na kubaini makosa katika uandishi, au pia kwa dawa ambazo zimekuwa zikitengenezwa na kampuni ya aina fulani unaweza kufahamu aina ya uandishi au alama zinazotumiwa na kampuni hiyo katika kifungashio. Hiyo itakuwezesha kubaini makosa endapo kuna mabadiliko ukilinganisha na alama uliyozoea kuiona awali.

Hayo ni baadhi ya mambo au vitu ambavyo unaweza kuvitumia kama viashiria vya kubaini bidhaa zisizo na ubora.

Baada ya kugundua viashiria hivyo katika dawa au bidhaa, ni muhimu kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) au mtaalamu wa afya katika kituo jirani cha kutolea huduma za afya ili kupata msaada na kutokomeza bidhaa husika.

Zipo sababu zinazochangia uwapo wa dawa au bidhaa zisizo na ubora sokoni, mojawapo ni wafanyabiashara kutokuwa waaminifu, ambao kwa makusudi hufanya hivyo ili kujiongezea faida.

Athari za dawa/bidhaa bandia kiafya ni pamoja na kusababisha usugu wa dawa, kuongeza gharama za matibabu kwa mgonjwa, kuleta athari za kiafya kwa mtumiaji pamoja na kuliingizia Taifa hasara kubwa ya manunuzi ya dawa na vifaa kwaajili ya wananchi.

Kutokomeza uwapo wa dawa na bidhaa zisizo na ubora ni jukumu la kila mmoja kwa kuwa wote ni watumiaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,044FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles