Na ASHURA HUSSEIN, MULEBA
MWANAFUNZI mmoja wa darasa la tano katika Shule ya Msingi ya Mtakatifu Joseph amefariki dunia na wengine 153 kujeruhiwa baada ya bweni walilokuwa wamelala kuwaka moto usiku wa kuamkia jana.
Shule hiyo ambayo ipo Rutabo Kamachumu wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, mabweni yake matatu yameteketea.
Tukio hilo lilitokea saa 9.00 usiku wa kuamkia jana.
Serikali wilayani hapa imesema imesikitishwa na ajali hiyo ya moto ikiwa ni miezi miwili tangu kutokea tukio jingine kama hilo shuleni hapo.
Tukio la wakati huo halikusababisha vifo isipokuwa mali za wanafunzi ziliteketea kwa kuwa tukio hilo lililotokea mchana.
Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango, ambaye alifika katika eneo la tukio usiku alisema Serikali itasimamia miundombinu ya shule hiyo ili majanga kama hayo yasiendelee kutokea.
Alisema katika tukio la jana mwanafunzi wa darasa la tano, Galatinus Godfrey ( 13 ) alifariki dunia baada ya kushindwa kupumua kwa vile bweni alilokuwa amelala lilizingirwa na moto mkubwa pamoja na moshi uliosababishwa ashindwe kujiokoa au kuokolewa.
“Nawapongeza wasimamizi wa watoto hao kwa jitihada za awali walizozifanya za kuokoaa watoto 153… siyo jambo rahisi, nawapongeza sana,” alisema.
Alisema jitihada za watumishi wa shule hiyo na wananchi wa jirani umekuwa msaada mkubwa kuwezesha kuzima moto huo usiweze kusambaa na kuleta madhara makubwa zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi, alithibitisha kutokea tukio hilo akiwa eneo la tukio.
Ollomi alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na sababu za ajali hiyo kutokea tena shuleni hapo ikiwa ni miezi miwili tangu tukio kama hilo kutokea na kusababisha bweni moja kuteketea na mali za wanafunzi.
Alisema wanafunzi hao ni wadogo wanahitaji utulivu katika kipindi hiki waweze kurejea katika hali ya kawaida na waweze kuendelea na masomo yao.
Wanafunzi wa darasa la saba ambao walikuwa wakiendelea na mtihani wa mock wamelazimika kusimamisha mtihani huo hadi kesho kutokana na hofu waliyo nayo.
Alisema katika uchunguzi huo watashirikiana na Kikosi cha Zimamoto na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), watumishi na wanafunzi .
“Chanzo cha moto huu hakijafahamika hivyo tutafanya uchunguzi wa kina kubaini kama kuna mtu au watu wanafanya hujuma au ni bahati mbaya pamoja na kudhibiti ajali kama hizo zisitokee tena.
“Tumeshaanza kupeleleza mashauri haya pia tunaomba ushirikiano kutoka kwa watumishi na majirani katika kutatua changamoto hii,”alisema kamanda.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Elias Kubigwa, alisema changamoto kubwa ya idara yake ni magari ya zimamoto.
Hata hivyo alisema serikali imejitahidi kutatua changamoto hiyo kwa kununua vifaa kwa ajili ya matengenezo ya magari ya idara hiyo mkoani Kagera.
Kubingwa alisema umewekwa mkakati wa dharura na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ili moto ukitokea watumie magari ya polisi ya washawasha kuzima moto.
Alisema uchunguzi wa tukio la moto uliotokea shuleni hapo Mei 12, mwaka huu ulibaini kuwa chanzo chake kilikuwa ni pasi ya mkaa iliyowekwa na mmoja wa wanafunzi wa bweni hilo chini ya uvungu wa kitanda ikiwa na mkaa wenye moto.
Alisema walitoa maelekezo kwa uongozi wa shule kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kunyooshea nguo na milango ya mabweni kufunguliwa kwa nje.
Vilevile walishauri ziondolewe nondo kwenye madirisha ili matukio haya yakitokea wanafunzi waweze kujiokoa jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.
Thamani ya mali zote zilizoteketea haijafahamika na mwili wa mwanafunzi aliyefariki dunia umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Kamachumu karibu na shule hiyo kusubiri maandalizi ya mazishi na wanafunzi walionusurika wanaendelea vizuri.