24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MWANAFUNZI MMOJA  AFARIKI, 153 WANUSURIKA   BWENI LIKIWAKA MOTO

 

Na ASHURA  HUSSEIN, MULEBA


MWANAFUNZI  mmoja wa  darasa  la tano  katika  Shule ya Msingi  ya Mtakatifu Joseph amefariki dunia na wengine 153 kujeruhiwa baada ya bweni walilokuwa wamelala kuwaka moto usiku wa kuamkia jana.

Shule hiyo ambayo  ipo   Rutabo Kamachumu wilayani Muleba Mkoa wa Kagera, mabweni yake matatu yameteketea.

Tukio hilo lilitokea saa 9.00 usiku wa kuamkia jana.

Serikali  wilayani hapa imesema imesikitishwa na   ajali hiyo ya moto ikiwa ni miezi miwili tangu kutokea tukio jingine kama hilo shuleni hapo.

Tukio la wakati huo halikusababisha vifo isipokuwa mali za wanafunzi ziliteketea  kwa kuwa tukio hilo lililotokea mchana.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba,   Richard Ruyango, ambaye alifika katika eneo la tukio   usiku alisema Serikali itasimamia miundombinu ya shule hiyo ili majanga kama hayo yasiendelee kutokea.

Alisema katika tukio la jana mwanafunzi wa darasa la tano,   Galatinus Godfrey ( 13 ) alifariki  dunia baada ya kushindwa kupumua kwa vile bweni alilokuwa amelala lilizingirwa na moto mkubwa pamoja na moshi uliosababishwa ashindwe kujiokoa au kuokolewa.

“Nawapongeza  wasimamizi wa watoto hao kwa jitihada za awali walizozifanya za kuokoaa watoto 153… siyo jambo rahisi, nawapongeza sana,” alisema.

Alisema jitihada za watumishi wa shule hiyo  na wananchi wa jirani     umekuwa msaada mkubwa  kuwezesha kuzima moto huo usiweze kusambaa  na kuleta madhara makubwa zaidi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustino Ollomi, alithibitisha kutokea  tukio hilo akiwa   eneo la tukio.

Ollomi alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi   kubaini chanzo na sababu za ajali hiyo kutokea tena  shuleni hapo ikiwa ni miezi miwili tangu tukio kama hilo kutokea na kusababisha bweni moja kuteketea na mali za wanafunzi.

Alisema  wanafunzi hao ni wadogo wanahitaji utulivu katika kipindi hiki  waweze kurejea katika hali ya kawaida na waweze kuendelea na masomo yao.

Wanafunzi wa  darasa la saba ambao walikuwa wakiendelea na mtihani wa mock wamelazimika kusimamisha mtihani huo hadi kesho kutokana na hofu waliyo nayo.

Alisema  katika uchunguzi huo watashirikiana na  Kikosi cha Zimamoto na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), watumishi  na wanafunzi .

“Chanzo cha moto huu hakijafahamika hivyo tutafanya uchunguzi wa kina   kubaini kama kuna mtu au watu wanafanya hujuma au ni bahati mbaya pamoja na kudhibiti  ajali kama hizo zisitokee tena.

“Tumeshaanza kupeleleza mashauri haya pia tunaomba ushirikiano  kutoka  kwa watumishi na majirani katika kutatua changamoto hii,”alisema kamanda.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Elias Kubigwa, alisema changamoto kubwa ya idara yake ni magari ya zimamoto.

Hata hivyo alisema  serikali imejitahidi kutatua changamoto hiyo kwa kununua vifaa kwa ajili ya matengenezo ya magari ya idara hiyo mkoani Kagera.

Kubingwa alisema umewekwa mkakati wa dharura na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ili moto ukitokea watumie magari ya polisi ya washawasha kuzima moto.

Alisema uchunguzi wa tukio la moto uliotokea shuleni hapo  Mei 12, mwaka huu ulibaini kuwa chanzo chake    kilikuwa ni pasi ya mkaa iliyowekwa na mmoja wa wanafunzi wa bweni hilo chini ya uvungu wa kitanda ikiwa na mkaa wenye moto.

Alisema walitoa maelekezo kwa uongozi wa shule kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kunyooshea nguo na milango ya mabweni kufunguliwa kwa nje.

Vilevile walishauri ziondolewe nondo kwenye madirisha ili matukio haya yakitokea wanafunzi waweze kujiokoa jambo ambalo halijafanyika hadi sasa.

Thamani ya mali zote zilizoteketea haijafahamika na  mwili wa mwanafunzi aliyefariki dunia umehifadhiwa katika  Kituo cha Afya Kamachumu   karibu na shule hiyo   kusubiri maandalizi ya mazishi na wanafunzi walionusurika wanaendelea vizuri.

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles