Na BENJAMIN MASESE
SERIKALI imeagiza uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza SekouToure kuhakikisha ofisa ustawi anakuwapo kwenye dirisha la matibabu kwa wazee kuwaondolea usumbufu kwa kupata vibali vya kuhudumiwa bure.
Agizo hilo lilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile alipotembelea hospitali hiyo kujionea jinsi huduma zinavyotolewa na kuzungumza na wagonjwa.
Dk. Ndugulile alisema pamoja na kuridhishwa na jinsi huduma zinavyotolewa katika hospitali hiyo ni lazima uwepo utaratibu mzuri kwa ofisa ustawi wa jamii apatikane maeneo ya huduma kwa ajili ya kutoa vibali vya huduma bure kwa wazee.
“Muweke utaratibu kuhakikisha wazee wanaokuja hawazunguki huku na kule kumtafuta ofisa ustawi wa jamii kwa ajili ya kuwaandikia vibali vya huduma bure.
“Hakikisheni anakuwapo hapa hapa wazee wasikae muda mrefu hospitalini na wapate huduma staiki,” alisema Ndugulile.
Mganga Mkuu wa Mkoa Dk.Rutachunzibwa Thomas, alimweleza waziri kwamaba kuongezeka kwa vituo vya afya vyenye nyota tatu kutoka kimoja mwaka 2015 hadi vituo 116 mwaka huu ni ushahidi wa kuimarika kwa sekta ya afya.
“Huduma imeimarishwa kwa sababu hata wiki iliyopita tulikuwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezindua Mpango wa Kuboresha Afya ya Uzazi kwa Wajawazito na Watoto (IMPACT) unaotekelezwa na Aga Khan Development, Network kwa ufadhili wa serikali ya Canada utakaogharimu Sh bilioni 25.
“Mpango huu unatekelezwa katika halmashauri zote nane za wilaya saba mkoani Mwanza… hii kwetu ni mafanikio makubwa,” alisema Dkt. Thomas.
Dk.Thomas alisema serikali imewezesha kupata asilimia 96 hadi 98 ya fedha ya dawa na vifaa tiba wakati awali walikuwa wakipata asilimia 46 tu.
Alisema ongezeko hilo limefanikisha kuboreha huduma ya afya huku akimkumbushia ahadi ya Mashine ya Mionzi (CT SCAN ) iliyoahidiwa na Waziri Ummy Mwalimu.
Alisema mpaka sasa chumba maalumu kwa ajili ya mashine hiyo kimeandaliwa kama alivyoagizwa na Serikali hivyo kinachosubiriwa ni mashine hiyo.
Dk. Ndugulile pia aliziagiza hospitali zote nchini kuepuka kuwaandikia wagonjwa dawa ambazo hazipatikani maeneo ya huduma kuepukana na usumbufu.