MADRID, HISPANIA
NAHODHA wa timu ya taifa ya Hispania, Sergio Ramos, amezungumza kwa mara ya kwanza tangu taifa hilo litolewe kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi huku akidai uongozi ulifanya makosa kumfukuza kocha.
Hispania ilimfukuza kocha wake, Julen Lopetegui, ikiwa ni siku mbili kabla ya timu hiyo kushuka dimbani katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Ureno.
Sababu za Lopetegui kufukuzwa ni baada ya klabu ya Real Madrid kuthibitisha kuwa kocha huyo atakuwa wao mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia na kuanza kwa msimu mpya wa ligi.
Nafasi yake ilichukuliwa na aliyekuwa mkurugenzi wa timu hiyo, Fernando Hierro, hivyo Hispania ambayo ilipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri ikajikuta inaondolewa kwenye hatua ya 16 bora dhidi ya Urusi bila ya kujali pasi zaidi ya 1,000 walizopiga.
“Tumetumia nguvu kubwa sana kwenye michuano hiyo, lakini ninaamini tumeondolewa kwenye michuano hiyo kutokana na mabadiliko ya uongozi yaliyofanyika, hiyo haikuwa mipango mizuri kwa ajili ya kutwaa ubingwa.
“Japokuwa tulijitahidi kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi ni kutokana na nguvu tulizozitumia, lakini ukweli ni kwamba tusingeweza kufika mbali,” alisema Ramos.